Serikali yaonya dhihaka kwa Rais

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameonya watendaji wa serikali wanaokataa kutekeleza maagizo ya viongozi wakuu akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na yeye.

Majaliwa alisema maagizo ya viongozi hao popote ni amri hivyo ni utovu wa nidhamu na dharau kwa mtendaji kutaka barua ili kuyatekeleza.

Ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusitisha kikosi kazi cha kodi, pia amesitisha kutumika kwa sheria ya usajili wa stoo na ameagiza apewe orodha ya mizigo iliyokamatwa na kuwekwa kwenye maghala ikiwamo ya wafanyabiashara kutoka nje ya nchi.

Majaliwa alitoa maagizo hayo Kariakoo, Dar es Salaam jana alasiri alipozungumza na wafanyabiashara na akawasihi wafungue maduka ili biashara ziendelee.

Hadi Majaliwa alipozungumza na wafanyabiashara hao, maduka Kariakoo yalikuwa yamefungwa tangu asubuhi.

“Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu popote wanapotamka jambo, linakuwa ni agizo na linapaswa kutekelezwa mara moja.

“Rais akisimama na kutupa maelekezo sisi wa chini yake tunapokea ni agizo na tunatekeleza mbiombio, mtendaji wa taasisi ya serikali hatekelezi anasema hajapewa barua?

“Mtu wa Kariakoo unatoa wapi barua ya Rais? Alafu unawaambia hilo ni agizo la kisiasa, hiyo ni dharau kubwa,” alionya.

Mei 12 wafanyabiashara Kariakoo walitangaza mgomo kuanzia jana wakidai kupinga urasimu uliopo bandarini, kamatakamata ya mizigo mitaani na sheria mpya ya usajili wa stoo.

Majaliwa kesho anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa makundi ya wafanyabiashara eneo hilo katika Ukumbi wa Anautoglo, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maagizo akiwa mkoani Kagera kuhusu masuala ya madai ya kodi za miaka zaidi ya mitano nyuma kwa TRA lakini hilo halijatekelezwa wanadai barua kutoka kwa Rais.

“Ndio sababu Rais Samia alikemea haya mambo akasema wafanyabiashara waachwe wafanye biashara kwa uhuru walipe kodi kwa hiari, sasa Rais hajatengua kauli hii hilo ni agizo lazima litekelezwe,” alisema Majaliwa.

Alimuagiza Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA asitishe kikosi kazi cha kodi hadi maelekezo mengine yatakapotolewa na kama kuna umuhimu, Waziri wa Fedha na Mipango ajulishwe na utaratibu maalumu utaandaliwa ili kuondoa manung’uniko kwa wafanyabiashara.

Aidha, alimwagiza Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA afuatilie kuona kanuni na sheria zipo na zinaelekeza vizuri namna ya kulipa kodi na akasema kama ni elimu haijatolewa vya kutosha kwa walipakodi waendelee kuelimishwa ili walipe kodi kwa hiari.

Aliagiza apewe orodha ya mizigo yote iliyokamatwa na kupelekwa kwenye maghala ya TRA kufanyiwa ukaguzi ili kero hiyo iangaliwe na kupatiwa ufumbuzi.

“Nimeambiwa hapa wateja wa nchi jirani wamepungua kwa sababu ya kamatakamata, sasa tukiendelea na mgomo kwa siku mbili tu, tunajiua na kuua soko letu.

“Sisi hatutakubali hilo, tunataka Kariakoo iendelee kuwa soko muhimu la bidhaa na wateja wanaofuata bidhaa kutoka nchi jirani waendelee kuja kwa wingi, vikwazo vyote tunaenda kuvizungumza tuvimalize,” alisema Majaliwa.

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alisema watendaji wote waliokejeli kauli ya Rais Samia kwa kusema ni ya kisiasa, Bunge litawaita Dodoma kuwashughulikia.

“Kejeli za kusema ni kauli za kisiasa ni kudharau mamlaka ya Rais, hawa Mheshimiwa Waziri Mkuu hatuwezi kuwaacha.

“Na sisi Bunge tuna sehemu yetu ya kulishughulikia, kuwaita watendaji wa serikali, kuwahoji na kuwachukulia hatua,” alisema Zungu.

Awali, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Martin Mmbwana alisema kero tatu walizozitaja ni za muda mrefu na wanaendelea kuumia.

“Tatizo la kwanza ni forodha, TRA wafanye makadirio yao kwa weledi na umakini. Lakini pia TRA wamegeuza Kariakoo shamba darasa, kila wakikaa wanawaza udhibiti kila siku wanakuja na jipya, wameajiri timu sita vikosi kazi tunanyonywa badala ya kufanya biashara kwa uhuru,” alisema Mmbwana.

Awali Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alikiri bungeni kuwa kuna mgogoro katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

————————————————————–

 

CCM yaonya wanaojipitisha

ubunge, udiwani-ANCHOR

Na Mwandishi Maalumu

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya wanachama wa chama hicho wanaoanza kujipitisha kwa wananchi ili kutaka nafasi za ubunge na udiwani.

CCM imeagiza wananchi hao waache mara moja kwa kuwa muda wa kufanya hivyo bado hivyo wanakiuka taratibu na miongozo ya chama.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisema hayo Bukombe jana wakati wa ufunguzi wa ukumbi wa mikutano wa CCM wilaya hiyo na kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya kupumzikia wageni.

Mradi huo umefikia asilimia 80 ya ujenzi na hadi sasa umegharimu zaidi ya Sh milioni 200.

“Mnakiuka taratibu na kwa kweli tunawaona na tutawachukulia hatua za kinidhamu.

“Chama hiki kina taratibu zake muda wa siasa bado sasa hivi waacheni waliopo wafanye kazi ikifika 2025 nafasi zitatangazwa hapo itakuwa ni ruksa kwa kila mwanachama kugombea ila kwa sasa acheni fitna na uchonganishi,” alisema Chongolo.

Aidha, aliagiza watendaji wa halmashauri nchi nzima wasimamie fedha za miradi ya maendeleo zilizopelekwa kwenye halmashauri zao, kwani serikali ya CCM imetoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha nchi inakua na maendeleo kwa wananchi yanaonekana.

“Serikali inadhamiria kuifungua nchi kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana sasa hatutakuwa na muhari wala haya kwa wale watakaochezea fedha hizo.

“Sisi kama Chama kinachotawala, tunataka kuona wananchi wanapata huduma safi kwa wakati, hivyo hatutakuwa na mchezo na yeyote atakayechezea fedha hizo,” alisema Chongolo.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko alisema Jimbo la Bukombe limetekeleza miradi ikiwemo ya afya, elimu na miundombinu kwa zaidi ya asilimia 80.

“Sisi kwetu kaulimbiu yetu ni kusema na kutenda na kupitia msemo huu tumeweza kushirikiana na kuhakikisha tunakamilisha miradi ya afya, miundombinu na elimu shule za msingi na kata tumeziboresha,” alisema Biteko.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Saidi Nkumba alisema mradi huo ulianza Julai 2019 sambamba na ujenzi wa ukumbi wa mikutano mradi huo ulihusisha ununuzi wa samani za ndani ya ofisi na ukumbi.

Alisema mradi huo ulihusisha pia ujenzi wa nyumba ya kupumzikia wageni, ujenzi wa jengo la migahawa, bustani kuzunguka eneo la ofisi, ukarabati wa vyoo matundu 6, ujenzi wa uzio pia ujenzi wa mtandao wa maji na tangi lenye ujazo wa lita 10,000.

—————————————————————————

 

Chalinze Cement yaishitaki

Brela kufutiwa leseni

 

Na Francisca Emmanuel

 

KAMPUNI ya Saruji ya Chalinze imefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Masijala Kuu Dar es Salaam, dhidi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ikipinga kufutiwa usajili wake.

 

Mkurugenzi wa kampuni hiyo na mwanahisa, Mohamed Bahadela akiwa mwombaji wa pili katika kesi hiyo namba 113/2023, pamoja na mambo mengine wameiomba mahakama iamuru kwamba mwombaji wa kwanza (Chalinze Cement) irejeshwe kwenye orodha za kampuni.

 

Pia waliomba mahakama hiyo itoe amri nyingine yoyote au afueni ambayo itaona inafaa kwa kuzingatia haki na usawa.

 

Katika hati ya kiapo iliyoandaliwa na waombaji hao chini ya Law Associates Advocates, wanadai kwamba Brela ndio yenye mamlaka ya kusajili na kuziondolea usajili kampuni nchini na ina jukumu la kutunza kumbukumbu zote za kampuni.

 

Wanadai kuwa kampuni ya Chalinze ilisajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kupewa namba za usajili 154321420 Desemba 3, 2021.

 

Wanadai kuwa kampuni hiyo ilisajiliwa kwa ajili ya kufanya biashara hususani katika uzalishaji, usafirishaji, uagizaji na uuzaji wa saruji, vifaa vya ujenzi na mashine.

 

Pia wanadai wana leseni ya uchimbaji kwa eneo ambalo wangefanyia shughuli zao na kwamba wamekuwa wakifuata sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira bila kusababisha changamoto au kutokuelewana kati yao na mamlaka za serikali.

 

Kampuni hiyo inadai kuwa wameshtushwa na taarifa za kufutiwa usajili zilizochapishwa na gazeti la Jamhuri Aprili 25, mwaka huu na kwamba katika taarifa hiyo ilionesha kwamba kampuni ilifutiwa usajili wake tangu Machi 3, mwaka huu.

 

Walidai baada ya taarifa hizo, walifanya ufuatiliaji na kubaini kwamba Brela imeondoa usajili wao na kuchapisha kwenye gazeti la Serikali Machi 3, mwaka huu.

 

Waliendelea kudai kuwa hawakuwa na taarifa wala notisi kuhusu kufutiwa kwao usajili licha ya kuendelea na shughuli zao za kila siku.

 

Wanadai kuwa kampuni hiyo inaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji kwa maendeleo kabla ya kufutiwa usajili.

 

Wanadai kuwa wamehuzunishwa na maamuzi ya Brela ya kuwaondolea usajili bila kuwapa notisi wala kuwasikiliza.

 

“Kwa hali ilivyo, madhumuni ya ombi hili ni kumuagiza Msajili wa kampuni kuirejesha kampuni hii ili aweze kuendelea kufanya biashara zake na shughuli nyingine zozote zinazolenga kukuza biashara na uwekezaji,” walidai.

 

Kampuni hiyo inahusishwa na kutotaka muunganiko wa kampuni za saruji nchini za Tanga na Twiga kuungana hivyo kukwamisha mchakato huo.

 

Muunganiko huo ulianza Oktoba 2021, wakati Scancem International DA (Scancem) ambayo ni kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG inayomiliki Twiga Cement na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement zilipotoa taarifa ya pamoja kuwa zimekamilisha masharti ambayo awali Twiga angepata asilimia 68.33 ya hisa kutoka Tanga Cement.

 

Tume ya Ushindani (FCC) iliidhinisha uamuzi huo, lakini ulibatilishwa na Mahakama ya Ushindani wa Haki (FCT) katika uamuzi wake wa Septemba 23, 2022, baada ya Kampuni ya Chalinze Cement Limited na Jumuiya ya Kutetea Watumiaji Tanzania (TCAS) kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

 

Hata hivyo, akielezea sababu za kufutwa kwa kampuni hiyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji alisema notisi ya kusudio la kufutwa kwa kampuni hiyo ilitolewa Januari 19, 2023, lakini hadi siku hizo zilipomalizika, hakukuwa na maelezo yaliyopokelewa.

 

“Anuani ya kampuni haipo kwenye usajili popote pale ndani ya Taifa kwa hiyo anuani ni ya uongo na hivyo huwezi kumfikia kwa sababu hujui yuko wapi anuani za wanahisa alizozisajili hazipo, kwa hiyo ni wakufikirika.

 

 

“Mawasiliano ya simu yaliyosajiliwa sio ya mwanahisa aliyetajwa kwenye kampuni hiyo,” alisema Dk Kijaji.

 

———————————–Mwisho—————————————

 

Habari Zifananazo

Back to top button