Waandishi HabariLEO wang’ara tuzo kupinga ukatili
WAANDISHI wa HabariLEO, Vicky Kimaro na Aveline Kitomari wameibuka vinara wa kupinga ukatili wa kijinsia na kutunukiwa tuzo zilizotolewa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF)
Waandishi hao wameibuka vinara kati ya watu 3,6000 waliowania tuzo hizo zilizofanyika usiku wa kuamkia jana Desemba 8, 2022 jijini Dar Es Salaam.
Vicky ameibuka kinara wa kutetea haki za afya ya uzazi na watoto, wakati Aveline amepata tuzo ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Akizungumzia mchakato wa kuwapata vinara 16 wa kupinga ukatili wa kijinsia, mmoja wa majaji katika tuzo hizo, Israel Hillunde, amesema mchakato wa kuwapata washindi hao ulikua mgumu.
“Hatua kadhaa zimefanyika hadi kuwapata washindi, kwanza sekretarieti ya Mkuki Coliation kupitia WiLDAF walikaa na kuweka vigezo,” amesema Hillunde.
Amesema kupitia vigezo hivyo walichambua na kupata watu watano katika kila kipengele na kupata jumla ya washindani 80.
“Tukachambua tena na kupata 48, hapa kazi ilikua ngumu, kazi zote zilikua bora, tukaangalia upekee, kisha tukachambua tena na kupata watu 16 ambao ndio vinara wetu wa leo,” amesema
Amesema vinara hao 16 sio watu mashuhuri, wanasiasa wala wabunge, ni watu tu wa kawaida ambao kupitia kazi zao wameweza kuleta matokeo chanya katika jamii.