ARUSHA: WATAFITI wameshauriwa kutumia maharage meusi kwa ajili ya kutengenezea mbegu za maharage ambayo hayasababishi gesi tumboni.
Ushauri huo umetolewa na Bwana Shamba kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Zakeo Bundara alipokuwa anatoa maelezo ya maharage hayo katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mimea Kimataifa iliyofanyika mkoani Arusha.
Amesema kwa maelezo ya wakulima wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, maharage hayo meusi yakipelekwa sokoni hakuna mtu anayetaka kuyanunua.
“Maharage hayo ni meusi kwa hali ya kawaida mtu anaweza asiyapende na yakipelekwa sokoni hakuna mtu anayeyataka.
“Sifa ya maharage haya hayasababishi gesi tumboni maana yake hayana kile kiambata cha sukari ambacho kinasababisha gesi tumboni.
“Maana yake kwa watafiti wanaweza wakafanya utafiti na kutengeneza mbegu za maharage ambazo hazisababishi gesi tumboni,” amesema.
Amesema mamlaka hiyo ina kitengo kinachotunza nasaba kwa ajili ya kutengeneza msingi wa kutengenezea mbegu bora.
“Hizi ni mbegu za kienyeji ambazo zimezoea mazingira yetu na zina sifa mbalimbali, ambazo ni msingi kwa ajili ya watafiti kuweza kuzalisha mbegu bora,” amesema.
Mbali na maharage meusi, amesema pia wana mbegu ya mtama wenye sifa ya kutoa kanyuzi pale inapotengeneza kichwa cha kutoa mbegu, ambapo ndege wanapotaka kushambulia wanakutana navyo vinawachoma hivyo wanaondoka.
“Pale kwenye mbegu mwishoni kuna kama kanyuzi na kwa sababu mtama unashambuliwa sana na ndege, wale ndege wanapoanza kushambulia wanakutana na vinyuzi nyuzi vinawachoma wanakata tamaa wanaondoka.
“Kwa hiyo inaweza ikawa ni sifa au tabia ambayo inaweza ikasaidia kwa zile aina zinashambuliwa sana ukazipa tabia hii maana yake tayari unakuwa umeshaimarisha afya ya mimea maana yake haishambuliwi na ndege,” amesema.
Ameeleza kuwa mpaka sasa wamekusanya zaidi ya sampuli 10,000 ambazo zipo kwa ajili ya yeyote atakayezihitaji wakiwemo watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu wanaozitumia kwa tafiti pamoja na taasisi kutoka ndani nan je ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Joseph Ndunguru amesema mamlaka hiyo ndio chombo mahiri kinachosimamia masuala ya afya ya mimea na viuatilifu hapa nchini.
Pia amesema mamlaka hiyo inahakikisha mimea na mazao yanakidhi matakwa ya masoko na mikataba ya kimataifa na kuweka mazingira salama kwa afya ya binadamu, wanyama na mimea kwa kuwa na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu nchini.