Tanzania yaimarisha uchumi jumuishi kwa kuzingatia makundi yote

DAR ES SALAAM:TANZANIA imeendelea kupiga hatua katika kujenga uchumi jumuishi unaowashirikisha watu wote, wakiwemo watu wenye ulemavu, kupitia uwekezaji katika huduma za afya, teknolojia saidizi, maji pamoja na mifumo ya ulinzi wa kijamii.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mratibu Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Susan Ngongi Namondo, wakati wa Mjadala wa Kitaifa uliojadili mwingiliano kati ya kazi za ulezi zisizolipwa na ukatili wa kijinsia nchini Tanzania.

Mjadala huo umeelekezwa katika kujenga mifumo jumuishi na inayobadili mitazamo ya kijinsia kuhusu kazi za ulezi kwa wasichana, vijana na wanawake wenye ulemavu.
Susan amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika kufanya maamuzi ili sera na mipango mbalimbali iweze kuandaliwa kwa kuzingatia mahitaji yao.

“Ujumuishaji wa watu wenye ulemavu haupaswi kuishia kwenye miundombinu au teknolojia pekee, bali pia ujengwe kupitia ushirikiano wa kijamii, fursa za kiuchumi na mifumo ya maendeleo inayowawezesha kuchangia katika ustawi wa taifa,” amesema Susan.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Watu Wenye Ulemavu, Ali Omar, amesema bado kuna changamoto kubwa zinazowakabili watu wenye ulemavu katika kupata huduma za kila siku, elimu, afya pamoja na kujitafutia kipato kutokana na mzigo wa kazi za ulezi zisizolipwa.

Amesema hali hiyo inaathiri ustawi wa wanawake, vijana na wasichana wenye ulemavu katika jamii.
Aidha, Omar amesema ripoti iliyowasilishwa katika mjadala huo itasaidia kupatikana kwa mwongozo bora wa kuboresha huduma na kuongeza uelewa kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Pia amewashukuru wadau mbalimbali, wakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wafadhili wa mradi huo, kwa kuendelea kushirikiana katika kuimarisha ustawi na haki za watu wenye ulemavu nchini.



