10 mbaroni kwa mauaji

MWANZA: Jeshi la polisi mkoani Mwanza limewakamata watuhumiwa 10 kwa mauaji ya Yumen Elias (54) aliyekuwa mlinzi katika eneo la Mwananchi lililopo Kata ya Mahina Wilaya ya Nyamagana na mkazi wa Nyashishi mkoani hapa aliyeuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 22, 2024 Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema kuwa mauaji hayo yalitokea Januari 16, 2024 majira ya saa tisa usiku na baada ya tukio hilo kuripotiwa kwa  jeshi la polisi uchunguzi wa haraka ulianza kufanyika na ilipofika Januari 18 mwaka huu jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti tofauti na maeneo tofauti.

“Watuhumiwa waliokamatwa ni Julias Joseph (22) mkazi wa Igoma, Paul John (23) mkazi wa Mwananchi, Leonidas Juma Bukwimba (19) mkazi wa Buhongwa,Abdullah Hassan (31) mkazi wa Nundu, Edward Boniface (19) mkazi wa Mahina,Mussa Robert (22) fundi magari mkazi wa Ilemela Kanisani,Steven Emmanuel (18) mkazi wa Nyakato Sokoni, George Mang’era Koloso (50) mfanyabiashara mkazi wa Nyegezi,Hamis Omary (21) mfanyabiashara mkazi wa Mabatini pamoja na Charles Chacha (27) mkazi wa Mahina Kati”……alisema  Kamanda Mutafungwa.

Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa ameeleza kuwa watuhumiwa hao wamehojiwa na uchunguzi unaendele kufanyika ili mashahidi waweze kupatikana kwaajili ya kukamilisha taratibu na hatua za kisheria za kuwafikisha mahakamani zifanyike.

Habari Zifananazo

Back to top button