Polisi Dar yamsaka mganga mwizi wa simu

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la mtu mmoja aliyejifanya mganga wa jadi maeneo ya Mji Mwema, Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwanywesha dawa inayodhaniwa kuwa ni  sumu na kuwalewesha watu 16 wa familia moja na baadaye kuwaibia simu.

Taarifa iliyotolewa leo Februari 20, 2024 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, ACP Muliro Jumanne Muliro imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Februari 18, 2024 kuanzia 3:00 usiku ambapo mtu huyo aliyejifanya mganga wa jadi  alipofika nyumbani kwa  familia ya Halisi Amani kwa lengo la kumtibia mke wake Fatuma Abdalla (52) aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo la miguu.

Aliwanywesha dawa iliyowalewesha familia nzima, wakapoteza fahamu na akawaibia simu tano za mkononi na kuondoka.

Aidha, kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtafuta mganga huyo  pia limemkamata kwa mahojiano mtu mmoja anayefamika kwa jina la Jalala Ally Said anayedaiwa kushirikiana na mganga huyo.

Pia amesema  wagojwa walilazwa na kupatiwa matibabu kwenye  Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni mpaka sasa wagonjwa 13 wamesharuhusiwa na wengine watatu waneendelea kupatiwa matibabu  na hali zao zinaendelea vizuri.

Tukio lingine limetokea Februari 9, 2024 eneo la Tuangoma, Mbagala ambapo mtu mmoja aliyejifanya mganga wa jadi aliwanywesha dawa zilizowalevya na baadae kupoteza fahamu watu watano na  kuwaibia pikipiki namba MC474, simu 3 za mkononi na Sh 30,000.

Jeshi la polisi linawatahadharisha wananchi kuhusiana na kuwepo kwa watu wanaojifanya waganga wa jadi  ambao huwalewesha watu na wanafamilia kwa ujumla na baadae kuwaibia.

Habari Zifananazo

Back to top button