75% wagonjwa wa kifafa hukimbizwa kwa ‘sangoma’

MILA potofu ikiwemo mapepo wachafu, masuala ya kishirikina yanachangia asilimia 75 ya watu wenye kifafa kupelekwa kwa waganga wa kienyeji badala ya hospitali.

Hayo yamesemwa leo Februari 12, 2024 na Mwenyekiti Chama cha Wanasayansi wa Magonjwa ya Mishipa ya Fahamu Tanzania (TNA), Profesa William Matuja katika Kongamano la maadhimisho ya siku ya kifafa duniani yanayofanyika Februari 12 kila mwaka duniani, kwa Tanzania yamefanyika katika ukumbi wa Ummy Mwalimu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Amesema, idadi kubwa ya watu nchini, wana imani potofu kuhusu kifafa, ambapo zaidi ya asilimia 36 bado wanaamini ugonjwa wa kifafa, unatokana na nguvu za giza matokeo yake zaidi ya asilimia 75 ya watu wazima na watoto wanaougua kifafa upelekwa kwa waganga wa jadi na viongozi wa kiroho kwanza, na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa matibabu ya kisasa hospitali.

Advertisement

Amesema, ugonjwa huo wa kifafa unatibika na kwamba kuchelewa kupatiwa matibabu kwa wakati husababisha ugumu kuudhibiti.

Anasema asilimia 26 ya wagonjwa wa kifafa wana matatizo ya kimwili kutokana na mshtuko wa moyo ambao haujatibiwa ikiwa ni pamoja na makovu mwilini, majeraha ya moto, mikazo, kuteguka kwa viungo hasa mabega, kuumia kichwa na vifo vya mapema.

Prof Matuja amesema, dalili za kifafa hutokea kwa sababu ya hitilafu za neva, ambazo hutokea ghafla na kuisha ghafla.

“Kifafa ni ugonjwa unaotokana na hitilafu au jeraha kwenye ubongo, linalosababisha mgonjwa kuanguka, kukakamaa kuzimia au kutokuzimia na wakati mwingine kutoa povu mdomoni,”amesema Prof Matuja na kuongeza

“Hitilafu inapotokea katika sehemu moja ya ubongo, hapa mgonjwa hapotezi fahamu ila anaweza kuwa hafahamu anachokifanya,” amesema.

Amesema watu wanaoishi na kifafa ni zaidi ya milioni 60 duniani kote. Kwamba Afrika ni bara ambalo limeathirika zaidi na tatizo la kifafa, ambapo katika watu 1,000, watu kati ya 20-50 wanaishi na tatizo hilo.