Suluhu changamoto kumi za biashara kwa wazalishaji dawa

DESEMBA 29 makala haya ya JOHN MAPEPELE chini ya kichwa cha habari: ‘Mwanga wa Matumaini Sekta ya Dawa Tanzania’ yalikuwa katika mtazamo wa kijamii yakiangalia malengo au sababu saba za Tanzania kukuza ujenzi wa viwanda vya dawa nchini.

Leo, yanajikita katika hotuba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alipozungumza katika Kikao cha Wazalishaji wa Dawa na Bidhaa za Afya Tanzania kilichofanyika Dar es Salaam Desemba 23, 2025 kwa mtazamo wa kiuchumi. Endelea…

Mchengerwa anasema serikali imekuja na Mkakati wa Kuharakisha Ukuaji wa Sekta ya Viwanda vya Dawa kwa kuwa inatambua maendeleo ya sekta katika viwanda vya dawa hayawezi kusubiri mifumo ya kawaida ya uamuzi inayochukua muda mrefu hadi kukamilika.

Kutokana na umuhimu wa kimkakati wa sekta hii kwa afya ya taifa, uchumi na usalama wa nchi, waziri huyo anasema serikali imeandaa na kuanza kutekeleza Mkakati wa Kuharakisha Uwekezaji Kwenye Sekta ya Dawa unaolenga kuondoa vikwazo vya kimuundo na kuharakisha uamuzi wa uwekezaji.

“Kupitia mkakati huu, serikali imejipanga kuweka mfumo maalumu wa uamuzi wa haraka kwa miradi ya viwanda vya dawa. Kupitia mfumo huu masuala ya leseni, vibali, ardhi, kodi, usajili wa bidhaa na upatikanaji wa miundombinu yatafanyiwa kazi kwa wakati mmoja badala ya kupitia hatua zinazojirudia ili kuhakikisha mwekezaji mwenye nia ya dhati anapata majibu ya wazi, ya haraka na yanayotabirika.

Kikosikazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (PIAT)

Ili kuhakikisha Mkakati wa Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa unatekelezwa kwa vitendo na kwa kasi inayolingana na umuhimu wa sekta hii, Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce -PIAT) kama chombo maalumu cha kufanya uamuzi haraka na kuratibu uwekezaji wa kimkakati katika viwanda vya dawa.

PIAT imepewa mamlaka ya moja kwa moja kufanya uamuzi wa haraka, kuratibu na kusimamia hatua zote muhimu katika mnyororo wa kuharakisha uwekezaji kuanzia tathmini ya mradi, vibali vya awali, uratibu wa taasisi husika hadi kufikia uamuzi wa mwisho wa utekelezaji.

“Hii inaondoa urasimu unaosababishwa na mizunguko mirefu ya maamuzi ya taasisi nyingi zisizoratibiwa,” anasema Mchengerwa na kuongeza: “Nguvu ya PIAT iko katika muundo wake. Wajumbe wake wakuu ni watu wenye mamlaka ya moja kwa moja ya maamuzi katika maeneo muhimu ya mnyororo wa uharakishaji wa uwekezaji wa dawa ikiwemo sera, udhibiti, fedha, ardhi, nishati, biashara, uwekezaji na ununuzi wa umma.”

Anaweka wazi: “Hii ina maana kuwa, maamuzi muhimu hayatasubiri rufaa au idhini za ziada, bali yatafanyika mezani kwa mtazamo mmoja wa kitaifa.” “Kupitia PIAT, serikali inajenga ‘strategic one-stop decision window’ (mfumo wa dirisha moja la kimkakati) kwa wawekezaji wa viwanda vya dawa, ambapo masuala yote yatajadiliwa na kuamuliwa kwa wakati mmoja, kwa uwazi na kwa muda uliobainishwa. Hii inaleta uhakika kwa mwekezaji na inajenga imani ya muda mrefu.

Zaidi ya hapo, PIAT ina jukumu la kufuatilia utekelezaji wa maamuzi kwa wakati halisi, kuhakikisha kila taasisi inayohusika inatekeleza wajibu wake ndani ya muda uliokubaliwa. “‘Taskforce’ (Kikosikazi) hii haifanyi maamuzi tu, bali inasimamia matokeo.”

Kwa ujumla, kuanzishwa kwa PIAT kunaashiria mabadiliko ya msingi ya namna Serikali inavyoshughulikia uwekezaji wa viwanda vya dawa kutoka uratibu wa kawaida kwenda katika uongozi wa kasi, wa mamlaka na unaolenga matokeo, unaoifanya Tanzania kuwa mazingira yanayovutia, yanayotabirika na yanayoshindana kimataifa katika sekta ya dawa.

Anasema: “Mabadiliko tunayoyazungumza leo si ya maandiko pekee, wala si ahadi za baadaye. Utekelezaji wake
umeshaanza na unaendelea kwa kasi… tayari serikali imechukua hatua katika muktadha huo.” Anaongeza: “Napenda kuwajulisha rasmi kuwa Tangazo la ‘Expression of Interest (EOI)’ (kutangaza nia) kwa ajili ya
uwekezaji katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya tayari limetolewa na kuchapishwa.”

EOI ni tamko rasmi la kuonesha nia ya kushiriki katika fursa ya kibiashara kabla ya kufanya mkataba kamili. EOI hutumika pale ambapo kampuni au taasisi inatangaza fursa kama zabuni, ubia, mradi au nafasi ya kibiashara kubaini mwenye nia kabla ya kuendelea na hatua rasmi kama zabuni au mkataba.

Kwa mujibu wa Mchengrwa, EOI hiyo inalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa, kuwezesha ubia kati
ya wazalishaji wa ndani na washirika wa kimataifa, kuleta mitaji, teknolojia na masoko pamoja na kuharakisha kufikiwa kwa viwango vya kimataifa, hususani WHO-GMP.

Anasema tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni Machi 2, 2026 ambao ni muda mahususi uliowekwa kuhakikisha mchakato unaendelea kwa kasi na uamuzi unapatikana kwa wakati. Katika kujibu hoja za wawekezaji na wazalishaji hao wa dawa, anasema zinagusa moja kwa moja gharama za uzalishaji, ushindani wa soko, mtiririko wa fedha, mazingira ya kisheria na uwezo wa viwanda kukua kutoka ndani kwenda nje ya nchi.

Kuhusu ukosefu wa ulinzi wa bidhaa za afya zinazozalishwa ndani dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, anasema serikali inatambua hitaji hili na imeanza kulishughulikia kama ilivyofanyika katika ununuzi wa majitiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Anasema: “Tunaelekea kufanya tena kwa bidhaa nyingine zaidi ya aina 20 kufuatia taarifa ya tathmini kukamilika, tutaielekeza MSD kununua nchini.”

“Kupitia PIAT nawaelekeza kufanya mapitio ya sera na mifumo ya kibiashara ili kuweka mazingira rafiki, ikiwemo kuimarisha matumizi ya upendeleo wa bei kwa wazalishaji wa ndani na kuhakikisha sera za ununuzi wa umma zinazingatia kipaumbele cha bidhaa za ndani pale ubora, viwango na bei shindani vinapokidhi matakwa ya nchi. Hii itahusisha pia kuwa na uwiano wa kiasi cha kununua nje na kununua ndani kulingana na uwezo wenu na mahitaji yetu kama nchi,” anaeleza.

Kuhusu ununuzi wa MSD kuzingatia zaidi bei ya chini, anasema serikali inafahamu changamoto hiyo. “Kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na mamlaka nyingine husika, tutaendelea kuboresha miongozo ya manunuzi ili bei isiwe kigezo pekee, bali izingatie pia ubora, uhakika wa upatikanaji, mchango wa kiuchumi na usalama wa dawa. Lengo ni kuhakikisha wazalishaji wa ndani wanapata nafasi stahiki katika soko la MSD,” anasema.

Anapozungumzia sheria ya manunuzi ya umma kuwa na ukomo wa malipo ya awali ya hadi asilimia 30  ikilinganishwa na wawekezaji wa nje wanaoruhusiwa kufungua hati kutoka benki inayomwahidi muuzaji kulipwa kwa niaba ya mnunuzi.

Kwa mujibu wwaziri wa afya, serikali inaendelea kutatua changamoto hiyo na kwamba, awali hakukuwa hata na hiyo asilimia 30 ya malipo ya awali.

“Tumeanza na hiyo na kwa kuzingatia mtiririko wa fedha kwa wazalishaji wa ndani. Tutajadiliana na taasisi husika ili kubaini namna bora ya kuboresha masharti haya bila kukiuka Sheria, ikiwemo matumizi ya mifumo mbadala ya kifedha itakayowezesha viwanda vya ndani kushiriki kikamilifu kwenye zabuni,” anasema.

Kuhusu madai ya kodi na gharama kubwa za maji na umeme, anasema serikali inatambua ukweli kuwa, gharama za nishati na maji zinaathiri gharama za uzalishaji na hivyo ushindani wa bei katika soko. Anaahidi: “Tutafanya majadiliano na wizara za sekta husika, kuangalia uwezekano wa kutoa motisha au ruzuku maalumu kwa viwanda vya kimkakati vikiwemo viwanda vya dawa ili kupunguza gharama za uzalishaji.”

Kuhusu wingi wa taasisi za ukaguzi na udhibiti, anasema PIAT itafanya utafiki na kutoa mapendekezo ya kuishauri Serikali namna bora ya kurahisisha na kuratibu mifumo ya udhibiti ili kupunguza taasisi za ukaguzi, gharama na muda unaotumika, bila kuathiri ubora na usalama wa bidhaa za afya. Mwandishi ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button