Abiria wakwama njiani zaidi ya saa 12

ABIRIA 49 wa basi la kampuni ya Makupa lenye namba za usajili T 958 DRK aina ya Sunlong, lililokuwa likisafiri kutoka Jiji la Arusha kuelekea Dar es Salaam, wamekwama kwa zaidi ya saa 12 katika eneo la Njia Panda, Himo wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya gari hilo kupata hitilafu njiani.

Wakizungumza na Daily News Digital, mmoja wa abiria, Ally Bilali, amesema basi hilo liliharibika majira ya saa kumi jioni, ambapo walitoa taarifa kwa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro.

Hata hivyo, waliambiwa kwa mujibu wa taratibu wanapaswa kusubiri kwa muda wa saa sita kabla ya hatua zozote kuchukuliwa.

Amesema baada ya muda huo kupita bila msaada wowote, baadhi ya abiria walilazimika kwenda kituo cha polisi Himo ambapo walipewa maelekezo na Inspekta Mayunga, hata hivyo hakuna msaada wa haraka uliopatikana.

“Tulielezwa kuwa askari angekuja kukagua gari lakini hakufika. Tumelala kwenye basi, wengine wamelazimika kulala hotelini. Mmiliki wa basi, dereva pamoja na kondakta hawatoi ushirikiano kabisa,” amesema Bilali.

SOMA: Latra kutoa vibali maalumu mabasi 150 Dar

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria, kampuni ilipaswa kuwarudishia nauli au kuwapatia usafiri mbadala.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyello, amesema taarifa hiyo wameipokea rasmi leo saa mbili asubuhi, na hatua zilianza kuchukuliwa mara moja.

Ameeleza kuwa dereva na kondakta walitoroka eneo la tukio, huku mmiliki wa basi alipofuatiliwa kwa njia ya simu hakutoa ushirikiano na baadaye simu yake haikupatikana.

Ameongeza kuwa hakuna abiria aliyewasiliana moja kwa moja na ofisi ya LATRA kuomba ufafanuzi wa kisheria, akisisitiza kuwa kwa mujibu wa taratibu, taarifa hutakiwa kutolewa kwa afisa mfawidhi wa mkoa.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa huo ACP Nassoro Sisiwayah, amesema wamefanikiwa kumkamata dereva wa basi hilo, Ibrahim Athumani, na kumshikilia mahabusu hadi mmiliki wa gari atakapopatikana.

“Tumechukua hatua kwa kuzingatia usalama wa abiria. Baada ya kulikagua gari hilo, tumebaini halikuwa salama kuendelea na safari. Tunawahakikishia abiria kuwa stahiki zao zitalipwa,” amesema ACP Sisiwayah.

Amesema basi hilo ni miongoni mwa magari yaliyopewa vibali vya muda na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa ajili ya kuhudumia ongezeko la abiria katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka mkoani Kilimanjaro.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I make up to $220 an hour working from my home. My story is that I quit working at Walmart to work online and with a little effort I easily bring in around $450h to $890h… Someone was good to me by sharing this link with me, so now I am hoping I could help someone else out there by sharing this link.Try it, you won’t regret it!.

    HERE→→→→→→→→→→ https://Www.Cash43.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button