Mwaka 2025 ulivyoing’arisha Tanzania kimataifa

DAR ES SALAAM; Mwaka 2025 utaendelea kukumbukwa kama kipindi ambacho Tanzania iliimarisha kwa vitendo nafasi yake katika diplomasia ya kikanda na kimataifa.

Kupitia mikutano ya ngazi ya juu, utekelezaji wa sera mpya ya mambo ya nje, ushiriki katika taasisi za kimataifa na ziara za viongozi, nchi ilijionesha kama mshirika wa kuaminika, mwenye dira ya maendeleo na ushawishi unaoongezeka.

Januari:Tanzania yaongoza ajenda ya nishati ya Afrika

Mwezi Januari, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Africa Mission 300, mkutano wa wakuu wa nchi, taasisi za fedha za kimataifa na washirika wa maendeleo uliofanyika Dar es Salaam.

Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kufikisha umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

Kwa kuandaa mkutano huo, Tanzania iliweka wazi msimamo wake kwamba nishati ni msingi wa maendeleo ya viwanda, ajira na ustawi wa kijamii, na kwamba diplomasia ya nishati ni sehemu ya mkakati mpana wa maendeleo ya taifa na bara.

Februari: Ushiriki wa Tanzania ajenda za Afrika

Mwezi Februari, Tanzania ilishiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliolenga masuala ya amani, usalama wa kikanda, mabadiliko ya tabianchi na mageuzi ya mifumo ya kifedha ya kimataifa.

Katika majadiliano hayo, Tanzania ilisisitiza mshikamano wa Afrika na umuhimu wa suluhu za Kiafrika kwa changamoto za bara, ikiendeleza msimamo wake wa kihistoria katika diplomasia ya bara.

Machi: Diplomasia ya afya yapata matokeo

Mwezi Machi, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg nchini Tanzania. Tangazo hilo lilitokana na tathmini ya juhudi za serikali katika kuzuia maambukizi, kuimarisha mifumo ya afya na kushirikiana na washirika wa kimataifa.

Hatua hii iliimarisha taswira ya Tanzania kama nchi yenye uwezo wa kitaasisi katika kudhibiti majanga ya kiafya na ikaiweka kwenye nafasi nzuri katika diplomasia ya afya ya kimataifa.

Aprili: Diplomasia ya utalii na uhusiano wa kimataifa

Mwezi Aprili, Tanzania iliandaa ziara maalum ya kidiplomasia kwa mabalozi na wawakilishi wa nchi za kigeni walioko nchini, waliotembelea vivutio vya utalii ikiwemo Serengeti, Ngorongoro na Zanzibar.

Ziara hiyo ililenga kuonesha mchango wa utalii katika uchumi wa taifa, uhifadhi wa mazingira na ujenzi wa mahusiano ya watu kwa watu, huku ikiimarisha utalii kama chombo cha diplomasia ya kiuchumi.

Mei: Prof. Janabi achaguliwa Mkurugenzi WHO

Katika Mkutano wa Afya Duniani (World Health Assembly) uliofanyika Geneva, Prof.  Mohamed Janabi wa Tanzania alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Faustine Ndugulile aliyefariki dunia mwisho mwa mwaka 2024,.

Uchaguzi huo uliwakilisha mafanikio ya kidiplomasia ya Tanzania na uliimarisha nafasi ya nchi katika maamuzi ya sera za afya ya umma barani Afrika.

Mei: Utekelezaji wa sera mpya ya Mambo ya Nje

Katika mwezi huo huo, serikali iliendelea rasmi utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2024, sera inayolenga kuoanisha diplomasia na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Sera hiyo iliweka mkazo katika diplomasia ya kiuchumi, afya, nishati na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi na diaspora katika masuala ya nje, ikiweka msingi wa diplomasia yenye matokeo yanayopimika.

Juni:  Tanzania yanyakua tuzo kimataifa utalii

Mwezi Juni, Tanzania ilitambuliwa kama Africa’s Leading Destination katika tuzo za World Travel Awards za kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi. Vivutio kama Serengeti na Zanzibar vilipata tuzo maalum, zikithibitisha ushindani wa Tanzania katika soko la utalii wa kimataifa.

Septemba; Tanzania katika Jukwaa la Umoja wa Mataifa

Mwezi Septemba, Tanzania ilishiriki Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, ikishiriki majadiliano kuhusu maendeleo endelevu, mageuzi ya taasisi za kimataifa na mabadiliko ya tabianchi.

Novemba;  Diplomasia ya Tabianchi

Mwezi Novemba, Tanzania ilishiriki katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP), ikisisitiza umuhimu wa haki ya nchi zinazoendelea kupata rasilimali na teknolojia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Desemba; Tanzania yapokea tuzo kimataifa

Mwisho wa mwaka, Tanzania ilipokea tena tuzo za kimataifa za utalii katika World Travel Awards Grand Final, ikithibitisha nafasi yake kama moja ya maeneo bora ya safari duniani.

Kwa jumla, mwaka 2025 ulikuwa mwaka wa utekelezaji wa diplomasia ya vitendo kwa Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button