Viongozi wa dini wahamasisha amani 2026

WAKATI mwaka mpya wa 2026 ukiingia, viongozi wa dini katika mahubiri ya kuukaribisha mwaka huu wamewataka Watanzania kumweka mbele Mungu na kufanya kazi kwa bidii pamoja na kulinda amani ya nchi. Sambamba na hilo, wamesema Mungu hajawapa kisogo mwaka 2025 licha ya changamoto zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi mkoani Kilimanjaro, Padri Prosper Siayako amewataka waamini na Watanzania wote kwa kuthamini neema ya Mungu aliyowajalia kwa kuuona mwaka mpya wa 2026, kwa kuwajibika ipasavyo ikiwemo kufanya kazi kwa bidii.

Padri Siayako alitoa wito huo wakati wa Ibada ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa 2026, iliyofanyika katika kanisa hilo Moshi mjini jana. “Ni jambo la kumshukuru Mungu kuuona mwaka mpya, ila kila mtu akumbuke ya kuwa kwa Mungu kukujalia kuuona mwaka mpya ana jambo na wewe na jambo hilo ni wewe kuwajibika ipasavyo kwa wito aliokujalia kuwa nao,” alisema.

Padri Siayako ambaye katika ibada hiyo aliwakilisha salamu za mwaka mpya wa 2026 kutoka kwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Ludovick Minde kwenda kwa waumini wa parokia hiyo, pia aliwaongoza waumini katika sala maalumu za kuombea familia, kanisa na taifa. Ametoa rai kwa waumini kuendelea kuliombea taifa ili amani iendelee kutamalaki nchini kutokana na umuhimu wake linapokuja suala la maendeleo.

Aidha, waumini wa Kanisa Katoliki kupitia Mkondo wa Kitume wa Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam wamehimiza Watanzania kudumisha amani, haki na bidii ya kazi. SOMA: “Amani ni kwa wote, hata wasiokuwa na vyama”

Aidha, wamemuomba Mungu na kuishauri jamii kuendelea kuomba ili mabaya yaliyojitokeza mwaka 2025 kwa taifa, yasijirudie tena. Wakihubiri kwa nyakati tofauti katika Ibada ya Mkesha wa Mwaka Mpya juzi katika viwanja vya Emaus, Ubungo, Dar es Salaam, Mwinjilishaji Epimark Mbeteni na Arbogast Kanuti walihimiza watu kudumisha amani, kumjua Mungu na kufanya kazi kwa bidii ili kupata matokeo makubwa.

Kanuti alihimiza amani na kuongoza maombi kwa taifa huku akihimiza watu kufanya kazi kwa bidii, kuondoa hofu ili kutenda makuu. “Kuna watu hapa watamuona Mungu wanayemwamini kwa namna ya tofauti mwaka 2026, mtafanya mambo makuu, kuweni tayari na hodari huku mkizidi sana kutafuta kumjua Mungu,” alisema.

Kwa upande wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwa’ichi alisema Mwaka 2025 Mungu hakuwapa Watanzania kisogo licha ya changamoto zilizotokea, akiwataka mwaka 2026 kuweka malengo safi na kusoma neno la Mungu. Ruwa’ichi alisema hayo wakati wa Misa Takatifu Mkesha wa Mwaka Mpya 2026 iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu juzi.

Amesema mwaka 2025 ulikuwa mwaka wa baraka na changamoto lakini licha ya changamoto hizo Mungu aliwapa Watanzania baraka katika maisha. Amesema Mungu amewapa watanzania zawadi ya huruma, na washukuru kwa zawadi ya uhai na baraka katika familia, uwajibikaji mahali pa kazi na mapito waliyopitia.

Amesema wanapouanza mwaka 2026 hakuna anayejua changamoto zinazokuja lakini Mungu yupo, akiwasisitiza Watanzania kujiaminisha na kujikabidhi kwa Mungu ili awe baraka katika maisha yao. Naye Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza amesema tangazo la serikali la Bima ya Afya Kwa Wote ni jambo la kumshukuru Mungu na kuliombea.

Ameeleza hayo jana katika ibada ya mkesha wa mwaka mpya iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front, Dar es Salaam. “Kuugua au kuuguza si kitu chepesi, inapotokea neema ya tangazo kama hilo ni la kuombea na kumshukuru Mungu kwamba watu wote wa juu, wa chini na wa kati wote wawe na bima ya afya ni jambo zuri sana,” alisema.

Ameeleza kuwa moja ya mambo ambayo Yesu anayafanya ni kujali afya za watu na kwamba kuhakikisha kujali afya za watu wote ni jambo la baraka. Lwiza aliongeza kuwa ni muda wa kutafakari mambo ambayo Mungu ameyafanya katika maisha yao ya kuwafanya kuwa na mioyo ya shukrani.

“Mungu anatafuta mtu mwenye moyo wa shukrani, ambaye atatafakari maisha yake yote, mtu mwenye moyo wa shukrani si mwenye fedha, mtu mwenye dhahabu, si mtu mwenye mali, shamba, ng’ombe bali anatafuta mwenye moyo wa shukrani si kwa sababu anavyo ni kwa sababu ndani ya moyo wake kuna neno la shukrani inayozidi vyote yaani mali, fedha na afya,” alifafanua.

Nao waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) wametakiwa kuanza mwaka 2026 kwa kulinda amani ya nchi na kanisa kwa kutenda matendo mema na kuyaacha matendo maovu waliyoyafanya mwaka 2025. Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG Ubungo Dar es Salaam, Paul Mulokozi alisema hayo jana wakati akihubiri kwenye ibada ya mkesha wa mwaka mpya 2026.

“Tukiwa tumenyooka mbele za Mungu, tukijitenga na uharibifu wa amani na kuondokana na yale aliyoyakataza Mungu katika maisha yetu tutafurahia baraka, mafanikio, ulinzi na tutapata yale mema na mafanikio ambayo Mungu amekusudia tuwe nayo katika maisha yetu ya hapa duniani,” alisema.

Amewataka waumini wa kanisa hilo kuanza mwaka vizuri kwa salama na amani ili wamalize mwaka vizuri kwa kufuata amri na neno la Mungu kwa sababu Mungu amewahesabia utakatifu hivyo mienendo yao iendane na kusudiao la Mungu. Pia, aliwasihi kuanza mwaka kwa kujiimarisha kiimani, kutubu dhambi zao zote na kuzishika amri za Mungu katika maisha yao ya mwaka 2026.

Ameongeza kuwa waumini hao hawapaswi kutoka mwaka 2025 kuingia 2026 wakiwa wana maovu kwa sababu ibilisi hawatakii mema ndio maana amekuwa akiwatumia watu wasio na hofu ya Mungu kuharibu maisha yao na amani ya nchi yao. Kutoka Dodoma, Askofu Mkuu wa Kanisa la Karmeli Assemblies of God Tanzania, Dk Evance Chande amewashauri viongozi wa dini kuacha mijadala ya kujadili imani za dini nyingine katika mitandao ya kijamii kwa kuwa inaweza kuliingiza, taifa katika machafuko.

Akiongoza ibada ya kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2026 iliyofanyika makao makuu ya kanisa hilo lililopo Ipagala jijini Dodoma, Dk Chande  amesema jamii ya Watanzania imeingiliana katika imani ya dini tofauti katika familia, ukoo na makazi na kusaidiana katika shughuli zote za kijamii. “Niiombe serikali kukemea mijadala hiyo inayofanywa kupitia kwenye mitandao ya kijamii kwani inaweza kusababisha kutoweka kwa amani ya nchi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button