Maridhiano, uchumi vyambeba Samia

WADAU mbalimbali wakiwemo wanasiasa, wasomi na wachumi wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kuliunganisha taifa kupitia Tume ya Maridhiano aliyoanza hatua ya kuiunda. Wamesema Rais Samia ni mfano wa kiongozi bora na kwamba hata tume atakayoiunda Watanzania watakuwa na imani nayo kwa jinsi muundo wake ulivyokuwa shirikishi.

Wakizungumza na HabariLEO jana, baadhi ya wanasiasa wamesema Rais Samia ni mfano wa kiongozi bora kutokana na kutowakatia tamaa wananchi wake kutokana na kushambuliwa kila kona. Mwanasiasa na mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Doyo Hassan Doyo alisema hotuba ya Rais Samia ya Mwaka Mpya inaonesha kuwa amedhamiria kuleta maridhiano ya kitaifa na kwamba mtu atakayekataa malengo ya hayo ni adui wa taifa.

“Rais amemaliza yote hakuna mjadala tena zaidi ya kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa mambo mazuri aliyowaahidi Watanzania,” alisema Doyo ambaye pia alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha NLD. Mbali na hayo, mwanasiasa Coster Kibonde alisema kupitia tume ya maridhiano itakayoundwa italisaidia taifa kuwa lenye umoja kwa kupata suluhu ya pamoja ambayo itakuwa mwafaka wa kuendesha taifa ili isirudi nyuma.

Ameshauri wakati wa uundwaji na utekelezaji wa tume hiyo kuzingatia uwepo wa makundi yote ikiwemo wanasiasa, vijana, wakulima na mashirika ya kiraia. “Atakapokuwa anaunda tume hiyo aguse kila sehemu ili hata tutakaposema hii ndio tume ya maridhiano ya kitaifa iwe inayoakisi uhalisi huo,” alisema Kibonde ambaye aligombea urais kupitia Chama cha Makini.

Amesema anaamini Rais Samia akishirikisha makundi yote italifanikisha taifa kusonga mbele kukuza uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja. Pia amempongeza Rais Samia kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwa na tume hiyo ambayo itakwenda kutibu kiu na majeraha ya Watanzania.

Kwa upande wake Mwajuma Milambo, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha UMD, amempongeza Rais Samia kwa kuliona hilo na kuiomba tume itakayoundwa iwe shirikishi kwa kuwashirikisha makundi yote hasa vijana kwa sababu wao ndio wajenzi wa taifa.

Ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati wa uundwaji na utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo katika kutafuta umoja, mshikamano na maridhiano ya kitaifa. Mhadhiri wa uchumi wa Chuo cha Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja alisema hotuba ya Rais Samia inaleta matumaini juu azma yake ya kuendeleza mikakati ya kukuza uchumi na kuleta maridhiano na umoja wa kitaifa katika siasa.

Amesema ameonesha nia ya kuendeleza maridhiano na mchakato wa katiba mpya kupitia Tume ya Maridhiano ambayo mchakato wake umeshaanza. Profesa Semboja aliongeza kuwa katika kukuza uchumi ni lazima mifumo ya sekta za maendeleo zifanyiwe maboresho kiuendeshaji kwa kuwa na viongozi wenye weledi, ujuzi na maarifa stahiki.

Amesema serikali inapaswa kutumia vyanzo vingine vya kuingiza mapato kando na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwemo kutumia rasilimali zilizopo nchini ikiwemo madini, ardhi, maji na rasilimali watu. “Nchi kama Tanzania tunatakiwa tuweze kutumia rasilimali zote tulizokuwa nazo watu, madini, ardhi tukitaka kuwa na maendeleo kwa nchi yenye rasilimali ni lazima kuzisimamia na kuziendesha wenyewe,” alisema.

Kwa upande wake Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Dk Isaack Safari amesema mwelekeo wa Tanzania kiuchumi ni mzuri na Rais Samia ana maono mazuri ambayo yanapaswa kuungwa mkono. SOMA: Rais Samia:Krismasi itukumbushe upendo

Amesema ukuaji wa uchumi kama alivyobainisha Rais Samia katika hotuba yake umechangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji na matumizi ya teknolojia bora na kwamba ubora wake unapaswa kuongezeka ili pato la taifa lizidi kuongezeka. “Pato linakuwa kwa sababu kuna wawekezaji, wanazalisha kwa wingi zaidi, lakini pia Watanzania wanaongeza juhudi, hivyo pato la taifa linaongezeka,” alieleza.

Mchambuzi wa uchumi, Ally Mkimo amesema ili uchumi uendelee kukua jitihada zinatakiwa kuongezeka katika kuwekeza katika sekta ambazo zimeajiri watu wengi kama kilimo na ufugaji na kuzifungamanisha sekta hizo na viwanda.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Really insightful post — Your article is very clearly written, i enjoyed reading it, can i ask you a question? you can also checkout this newbies in seo. thank you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button