Samia akabidhi zawadi kwa wahitaji

WAKATI Watanzania wakiungana na watu wengine duniani kote kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2026, Rais Samia Suluhu Hassan amekabidhi zawadi mbalimbali za mwaka mpya kwa watu wenye mahitaji mkoani Kilimanjaro. Zawadi hizo zilikabidhiwa juzi kwa wahitaji hao na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa zawadi hizo, Nderiananga ametoa wito kwa jamii kuwapenda, kuwajali na kuwahudumia makundi ya wenye mahitaji maalumu ili kukuza umoja na mshikamano katika jamii. Nderiananga alisema zawadi hizo zimeenda kwa watoto 190 wanaolelewa katika Kituo cha The Creator Share kilichopo Kata ya Kirua, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Zawadi hizi ni sehemu ya utaratibu wa Rais Samia kutoa zawadi za sikukuu na leo hii (juzi) niko hapa kutekeleza utaratibu huo katika kusherehekea Mwaka Mpya wa 2026,” alisema. Nderiananga alisema ndani ya siku 100 tangu alipoanza kipindi cha pili cha uongozi wake, Rais Samia ameendelea kuleta faraja, upendo, tumaini na umoja kwa Watanzania huku akisema kuwa kitendo hicho ni ishara ya upendo mkubwa alionao kwa wananchi bila kujali hali zao za kimaisha.
Amezitaja zawadi alizokabidhi ni mchele kilo 100, ngano kilo 50, mbuzi wawili, sabuni, mafuta ya kupikia, madaftari, sukari kilo 25 na vinywaji laini aina mbalimbali. Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema ili kuwa na ustawi wa maisha ya kijamii ni lazima kuwajali watu wenye uhitaji ili waweze kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
Akipokea zawadi hizo, Ofisa Rasilimaliwatu katika kituo hicho, Judith Shio amemshukuru Rais Samia kwa moyo wa upendo alionao kwa watu wenye mahitaji maalumu ambapo alitoa wito kwa wadau kujitolea ili kuendelezwa moyo wa upendo na faraja kwa makundi hayo. SOMA: Friends of Kagera waamua kugusa maisha ya wahitaji



