Wagonjwa TB walioacha dawa kusakwa

WILAYA ya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia Idara ya Afya imeanza msako wa kuwatafuta wagonjwa wa Kifua Kikuu waliokatisha matumizi ya dawa ili waendelee kunywa, ikiwa ni mkakati wa kumaliza tatizo hilo na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Msako huo unaoongozwa na Mratibu wa Kifua Kikuu na ukoma wa Wilaya ya Tunduru, Dk Mkasange Kihongole unawashirikisha viongozi wa serikali za vijiji na umewezesha kuokoa watu kadhaa ambao walisitisha matumizi ya dawa, hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza maisha. SOMA: Tanzania yatajwa maambukizi ya TB

Akizungumza na wazazi katika Kijiji cha Nandembo, Dk Kihongole alisema msako huo unalenga wale wote waliobainika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo, wakiwemo watoto wadogo walioibuliwa kupitia kampeni ya uchunguzi wa vimelea vya TB katika maeneo mbalimbali na walianzishiwa dawa lakini waliamua kukatisha.

Dk Kihongole amesema serikali inatumia fedha nyingi kuagiza dawa kwa ajili ya watu wanaobainika kuugua Kifua Kikuu, hasa ikizingatia kuwa ugonjwa huo ni kati ya magonjwa 10 duniani yanayoongoza kuuwa watu wengi na Tunduru ni kati ya wilaya iliyoathirika sana maradhi hayo.

Amesema madhara ya kukatisha kunywa dawa ya Kifua Kikuu ni kubwa, kwani mgonjwa mwenye homa hiyo asiyepata tiba sahihi anaweza kuambukiza watu wengine zaidi ya 15 kwa wakati mmoja, ndiyo maana serikali imeweka utaratibu wa kutoa dawa za ugonjwa huo bure.

Kwa mujibu wa Dk Kihongole, mtoto kukaa mbali na huduma za afya ni unyanyasaji, kumnyima haki na ukatili dhidi ya mtoto. Vilevile, kutompatia dawa mtoto mwenye maambukizi ni kukiuka Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009.

“Mzazi anayejua mtoto wake amepata ugonjwa lakini hampeleki kwenye matibabu ni kosa kisheria na kuna adhabu ambayo muhusika atakabiliana nayo. Nasisitiza wazazi na walezi wahakikishe wanawapeleka wagonjwa kwenye maeneo ya kutolea huduma ili wapate tiba sahihi na kufuatilia hali ya afya zao,” alisema.

Dk Kihongole amesema Kifua Kikuu kinatibika kwa mgonjwa kutumia dawa kwa miezi sita bila kukatisha na idara ya afya kupitia Kitengo cha Kifua Kikuu na Ukoma inaendelea na kampeni ya uchunguzi na kutoa elimu kwa jamii ili wafahamu chanzo, madhara, tiba na hatua ya kuepuka kupata Kifua Kikuu.

Mmoja wa watu wanaofanya kazi ya kukusanya sampuli za makohozi na kupeleka hospitalini kwa ajili ya uchunguzi katika Kijiji cha Nandembo, Joseph Hyera alisema katika kampeni ya Juni mwaka huu, watu 12 waligundulika kuwa na Kifua Kikuu katika kijiji hicho.

Kati yao, watu watano walifuatilia matumizi sahihi ya dawa, sita hawakuwa makini na mgonjwa mmoja alikimbia, hivyo jitihada za kumtafuta zinafanyika ili aweze kuendelea kunywa dawa. Mkazi wa Kijiji cha Nandembo, Omari Mkumbi amepongeza jitihada za muda mrefu zinazofanywa na hospitali ya wilaya chini ya kitengo cha Kifua Kikuu na ukoma, kufanya kampeni ya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na watu wazima katika maeneo mbalimbali.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button