REA yazindua kituo cha kusambaza umeme Mtera

DODOMA: Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua kituo cha kupoza na kusambaza meme cha Mtera (2x10MVA, 220/33kV), ambacho kimeongeza ubora wa umeme.
Hatua hiyo imepunguza changamoto za ‘voltage’ ndogo na kuboresha huduma za kijamii, afya, elimu, maji na mawasiliano katika mikoa ya Iringa na Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo Januari 16, 2026 katika eneo la bwawa la Mtera, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema upanuzi wa kituo cha Mtera ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu vijijini.
Kituo cha Mtera kimejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 9.7 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia REA na Serikali za Sweden na Norway.

Kituo hicho kitawanufaisha wananchi wa wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma pamoja na wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, kwa kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Waziri Ndejembi aliashiria kuwa kati ya vitongoji 64,352 nchini, bado vitongoji 21,000 havijapatiwa umeme. “Kwa maagizo ya Rais Samia, ndani ya siku zake 100 za uongozi wake ni kuhakikisha umeme unaifikia vitongoji hivyo. Kufikia 2030, tunatarajia vitongoji vyote nchini vitakuwa vimeunganishwa na umeme,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi wa Dodoma na Iringa kujitokeza kuomba kuunganishiwa na umeme huo wa uhakika ili kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na upatikanaji wa nishati. “Umeme upo wa kutosha, niwaombe wananchi wajitokeze,” alisema Ndejembi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kituo cha Mtera kimepunguza kwa kiasi kikubwa matatizo kwa wananchi waliokuwa wakikabiliana na changamoto ya umeme dhaifu kwa miaka sasa sasa wamerahisikiwa, kwa kuwa kituo hiki kinatoa suluhisho la muda mrefu la upatikanaji wa umeme.



