Tanzania kujitosheleza uzalishaji dawa ifikapo 2030

DAR ES SALAAM: WAZIRI Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema Taifa limejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, kiwango cha uzalishaji wa dawa kuongezeka kutoka asilimia 10 ya sasa hadi kufikia asilimia 65 .
Akizungumza katika Kongamano la Wazalishaji wa Dawa pamoja na Vifaatiba jijini Dar es Salaam, amesema uhamasishaji wa wawekezaji wa viwanda vya dawa nchini ni mpango wa Taifa ulioanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, shabaha ikiwa ni kuona Tanzania inajitosheleza kwa bidhaa hiyo lakini pia kuwa muuzaji kwa nchi zingine ifikapo 2030.
“Huu ni mpango wa Taifa uliowekwa wazi ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuhakikisha nchi inakuwa na uhuru wa kuzalisha dawa zake yenyewe,” amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema wamepata wadau wa uwekezaji zaidi ya 40 kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Ujerumani, Uingereza, Marekani na India, ambao watahakikisha changamoto zote zilizokumba sekta ya uzalishaji wa dawa zinatatuliwa kwa sababu wamejipanga vizuri.
Aidha Waziri Mchengerwa amesema kuwa kwa mipango hiyo ya Wizara ya Afya, Taifa litapiga hatua katika uzalishaji wa dawa ndani ya nchi, jambo litakalookoa fedha za Serikali zinazotumika kuagiza dawa nje ya nchi na pia kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wananchi.
.-



