Waathirika vurugu za uchaguzi kutibiwa kisaikolojia

TUME ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imesema itawapatia waathirika wa vurugu hizo huduma ya kisaikolojia kutokana na madhila za vurugu hizo kwa kuwakutanisha na wataalamu wa saikolojia.
Baadhi ya waathiriwa waliofika na kutoa ushahidi wao ni waliojeruhiwa kwa risasi katika miili yao huku wengine wakiwa na ulemavu wa kudumu.
Mjumbe wa tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue ambaye anaongoza mikutano ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, alisema hayo wakati tume hiyo ikipokea ushahidi kutoka kwa makundi mbalimbali ya waathirika wa vurugu hizo katika Ukumbi wa Karimjee.
Makundi ya waathirika waliotoa ushahidi wao ni kundi ambalo ndugu zao walipoteza maisha, kundi lililopoteza ndugu zao na hawajui walipo, kundi la watu waliopata ulemavu na kundi la watu waliopoteza mali zao.
Balozi Sefue alisema baadhi ya wananchi waliopata ulemavu wa kudumu kutokana na vurugu hizo wanahitaji kupata ushauri wa kisaikolojia ili waikubali hali hiyo na maisha yaendelee na kwamba tume inatoa msaada wa kisaikolojia kwa kuwakutanisha na wataalamu hao.
Baadhi ya waathiriwa waliopata majeraha na ulemavu wa kudumu waliiambia tume kuwa kutokana na ulemavu huo walioupata wakiwa katika shughuli zao halali, walifikia hatua ya kukata tamaa ya kuishi.
“Hatuna uwezo wa kuwapatia miguu bandia lakini tunaweza kuwatafutia wataalamu wa saikolojia na kuwaunganisha na ninyi ili muweze kupata huduma hiyo na maisha yaendelee,” alisema Balozi Sefue.
Aidha, aliwasihi wananchi wanaofika kutoa ushahidi wa kitu gani kilitokea siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wasiwe na wasiwasi na kwamba maswali wanayoulizwa yanalenga kupata ukweli wa taarifa zinazotolewa.
Kadhalika, wananchi ambao biashara zao ziliathirika kutokana na vurugu za uchaguzi wameiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili wahudumie familia zao kwa sababu mali zao ziliporwa na watu walioshiriki vurugu hizo.
“Biashara zangu zilizoharibiwa katika eneo la Buguruni, thamani yake inafika Shilingi milioni 42, naiomba serikali iangalie namna ya kunisaidia kwani sasa hivi nina miaka 53 nguvu za kutafuta na kuijenga biashara hii sina tena,” alisema mwananchi aliyepoteza maduka yake mawili Buguruni.
Mwananchi mwingine ambaye ni kiongozi katika ngazi ya Shina Mtaa wa Tabata, ameishauri serikali kuchukua hatua mapema baada ya kujitokeza viashiria vya uvunjifu wa amani ili kuokoa maisha na mali za wananchi.
Alisema kwa kuwa maandamano ni tiba ya mioyo ya watu, serikali iangalie namna ya kukaa na vijana katika zama hizi za kidijiti ili kujua mambo wanayowaza ama kuyatekeleza katika kujenga mustakabali wao au wanaotaka watekelezewe ili kuwa vijana wema kwa maslahi ya taifa.
“Serikali imetenga asilimia nne ya mikopo ya halmashauri kwa ajili ya vijana lakini ukifuatilia kwa undani hutakuta kijana hata mmoja aliyepata mikopo hiyo. Waziri wa Vijana atafute jukwaa la kukutana na vijana ili kujua hali halisi ya vijana na achukue hatua ili vijana waweze kuwafikia vijana,” aliongeza mwananchi huyo.



