Kasekenya aridhishwa makandarasi wazawa

SHINYANGA: NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameridhishwa na kazi zinazotekelezwa na makandarasi wazawa waliokuwa wakijenga madaraja matatu yaliyogharimu zaidi ya Sh billioni 13.5 fedha kutoka ufadhili wa Benki ya Dunia katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Mhandisi Kasekenya amesema hayo kwenye ziara yake ya siku moja ya ukaguzi wa madaraja hayo yaliyotokana na mradi wa dharura huku akieleza makandarasi wameonyesha ujenzi wa kiwango cha juu tofauti na miaka ya nyuma.

Amesema serikali itaendelea kuboresha na kujenga miundombinu mbalimbali ya barabara na madaraja na maeneo yaliyokuwa korofi ili kuwaondolea kero wananchi. Imeelezwa kabla ya kujengwa madaraja hayo wananchi walikuwa wakiteseka kipindi cha masika kwa kutoa pesa na kuvushwa.
“Tunamshukuru Rais kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hii kwa wakandarasi wazawa hivyo nasi tunataka waendelee kupewa kazi sababu madaraja yote yamekamilika na fedha zote wamelipwa,” amesema Mhandisi Kasekenya.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya amesema kabla ya ujenzi wa madaraja hayo matatu ambayo miundombinu yake iliharibiwa na mvua nakuanza kazi ya kuirejesha kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia Novemba mwaka 2024 hadi Januari 2026 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 99 ikiwa bado sehemu za kingo wanakamilisha na kazi ndogondogo.
“Madaraja hayo ni Kasenga lililokuwa na urefu wa mita 80 lililogharimu ya Sh bilioni 5.1, na Ng’hwande mita 60 lililogharimu zaidi ya Sh bilioni 4.2 yote yalikuwa yakitekelezwa na kampuni ya Jonta Investiment Ltd na daraja la Ubwagwe lililogharimu zaidi ya Sh bilioni 4.1 lililotekelezwa kutoka kampuni ya Salum Motors Transport Co.Ltd katika halmashauri ya Ushetu,”amesema Mhandis Mwaikokesya.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Jonta Investment, John Ntalimbo alisema wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoka fedha hizi kwa wakandarasi wazawa hivyo wamewaamini na wao kuaminika nakuomba bajeti iongezwe ya utekelezaji miradi.
Ntalimbo amesema wasimamizi wamekuwa wakitoa ushirikiano ulio bora na sasa wanajivunia kushindanishwa na wakandarasi wageni katika kuomba kazi kwani wameiva kwa kiwango kikubwa walichojifunza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya madaraja.
“ Kwa wakandarasi wazawa tunaendelea kusonga mbele kwani walitujaribu na tumetekeleza kwa ujasiri mkubwa na mioyo yetu imeridhika na miradi hii tunaikabidhi”amesema Ntalimbo.



