Minara 1,041 imejengwa ndani ya miaka 4

DODOMA; SERIKALI imesema katika kipindi cha miaka minne jumla ya minara 1,041 imejengwa na inatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Mwawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Switbert Mkama ametoa kauli hiyo bungeni leo Februari 2, 2026 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini, Fadhili Chilombe aliyehoji serikali ina mkakati gani wa kujenga mnara wa mawasiliano katika Vijiji vya Kazamoyo, Imani na Kilimani katika Jimbo la Tunduru Kusini.
“Katika kipindi cha miaka minne jumla ya minara 1,041 imejengwa na inatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi,” amesema na kuongeza kuwa kati ya minara hiyo, minara 758 imejengwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigitali ambao ulizinduliwa rasmi na Rasi Dk Samia Suluhu Hassan, Mei 13, 2023.
“Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na jitihada za kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyosalia ambapo tarehe 05 Desemba, 2025 mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 201 ilisainiwa, na utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2027.
“Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2025/26, Serikali kupitia UCSAF imepanga kufikisha huduma hizo katika maeneo mengine 280, yakiwemo maeneo ya kimkakati kama vile reli ya kisasa (SGR), hifadhi za Taifa, barabara kuu na maeneo ya mipakani.
“Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zake na makampuni ya simu, inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Miaka Mitano (2025–2030) wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu wenye lengo la kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini,” amesema Naibu Waziri.


