TRA yazionya bandari kavu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itawachukulia hatua za kisheria wamiliki wa kampuni za bandari kavu zinazochochea ukwepaji wa malipo ya ushuru wa forodha. Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alitoa onyo hilo alipofanya kikaokazi na wamiliki wa kampuni hizo mkoani Dar es Salaam jana. “Nataka mfanye kazi saa 24, baadhi ya ICD ambazo zinachochea ukwepaji wa kodi au mazingira hayo, tutawachukulia hatua za kisheria,” alisema Mwenda.

Aidha, amesema lengo la mkutano huo ni kujadiliana namna ya kuboresha utendaji na kuimarisha ushirikiano kati yao ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo. “TRA tunawathamini na tutaendelea kuwapa ushirikiano katika kuongeza ufanisi,” alisema Mwenda.

Amesema idara ya forodha na TRA hawawezi kufanya kazi zao kwa ufanisi kama bandari kavu hazitatimiza wajibu wao wa kulinda usalama wa bidhaa ambazo haziruhusiwi kuingia nchini. Mwenda aliagiza wamiliki wa kampuni za bandari kavu kuweka utaratibu wa kukutana na TRA mara nne kwa mwaka ili kujadili changamoto na mafanikio ya utendaji kwa ushirikiano huo.

Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA, Juma Hassan alisema ufanisi wa forodha unategemea ufanisi wa bandari kavu kwa kuzingatia kuwa sekta ya bandari kavu inashusha mizigo mingi iliyopita katika Bandari ya Dar es Salaam na kuchangia asilimia kubwa ya Pato la Taifa.

“Katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa miezi sita idara ya forodha ilitakiwa kukusanya Shilingi trilioni 6.8 lakini ilikusanya trilioni 6.9, ongezeko la asilimia moja na katika fedha hiyo asilimia 52 ilitokana na makusanyo ya mzigo inayopita bandari kavu,” alisema. Aidha, kwa upande wa chama cha wamiliki wa bandari kavu waliomba yafanyike maboresho kwenye mifumo kukabiliana na changamoto kubwa wanazokutana nazo kwenye utendaji wao.

Changamoto hizo ni pamoja na utolewaji wa leseni ya biashara kwa mwaka mmoja, muda ambao hautoshelezi upande wa mifumo ya ubebaji wa mizigo na kunasa kwa magari ndani ya bandari. SOMA: Chongolo aomba bandari kavu Makambako

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button