Lishe endelevu yawafikia wakulima Iringa

MRADI wa USAID Lishe Endelevu umeanzisha mashamba ya mfano 186 na kuwafikia na kuwajengea uwezo wakulima 6,842 ikiwa ni sehemu ya mikakati yake ya kuusaidia Mkoa wa Iringa kukabiliana na udumavu.
Takwimu za mwaka 2018 zinaonesha katika kila watoto 100 wenye miaka chini ya mitano mkoani humo, 47 sawa na asilimia 47 wamedumaa kutokana na lishe duni.
Mratibu wa USAID Lishe Endelevu (Kilimo Mifugo na Uvuvi), Samwel Kitila alisema hatua hiyo imelenga kuiwezesha jamii kuongeza uzalishaji na ulaji wa vyakula vyenye virutubishi vingi.

Alisema mradi haukuishia kwa wakulima kwani ulifanya pia kazi ya kuvijengea uwezo Vikundi 99 vya kuweka na Kukopa(VSLA) ili viwe na sifa ya kupesheka na tayari 50 kati yake vimefanikiwa kupata mkopo wa Sh Milioni 83 ili kuendelea kukuza shughuli zao za kijasiriamali.
“Mradi pia umedhamiria kuongeza upatikanaji na utoaji wa huduma bora za lishe katika ngazi ya vituo vya afya na jamii kwa kuimarisha uwezo wa watoa huduma za afya,” alisema.
Katika kikao cha pamoja cha wadau kilicholenga kujua mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo, changamoto na utatuzi wake ili kuweka mikakati endelevu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Leonard Masanja aliwataka viongozi na watendaji wa mkoa kushirikiana na wadau ili kupunguza udumavu mkoani humo.

Mhandisi Masanja alisema; “Kila mmoja wetu anatakiwa kuhakikisha anatoa huduma bora za lishe na kuwafikia walengwa wote ili kupunguza athari za utapiamlo na hasa udumavu miongoni mwa jamii yetu.”
Kwa kupitia msaada wa Watu wa Marekani, Masanja alisema mkoa wa Iringa unatambua mchango mkubwa wa Mradi wa USAID Lishe Endelevu wa mwaka 2018 hadi 2023 katika kutatua tatizo la lishe duni, utapiamlo.
Alisema mradi huo umechangia katika maeneo mengi yakiwemo; kuongeza hamasa ya mabadiliko ya tabia kwa wanawake wajawazito, wanaonyonyesha, watoto walio chini ya miaka mitano na vijana wa rika balehe kwa kupitia wanawake vinara, vikundi malezi na klabu za lishe.
Pia amewasihi watendaji kusimamia mipango na bajeti za lishe kwa mwaka 2023/2024 kuanzia ngazi ya kijiji hadi halmashauri ili kuhakikisha shughuli zilizopangwa zinaendelea kutatua changamoto za lishe zilizopo katika jamii.
“Vituo vyote vya kutolea huduma za afya, shule na serikali zipange shughuli za lishe zitakazosaidia kupunguza utapiamlo,” alisema Masanja.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Lishe Endelevu Tanzania Dk Joyceline Kaganda, Dk Benny Ngerez alisema mbali na Iringa, mradi huo wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa ya Rukwa, Morogoro na Dodoma.



