Programu kuharakisha mfumo ubunifu yazinduliwa

DAR ES SALAAM; TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Sahara Ventures, imezindua rasmi programu ya kitaifa ya kuharakisha ukuaji wa biashara changa na kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini (Tanzania Ventures Lab).
Mfumo huo utalenga kuunganisha wabunifu, watafiti, wawekezaji kutoka sekta binafsi, na taasisi za serikali ili kuboresha uhusiano wa kijamii na kiuchumi kwa wadau hao.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo, Machi 12, 2026 makao makuu ya COSTECH jijini Dar es Salaam na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za serikali, vyuo vikuu, vyuo vya ubunifu, sekta binafsi, wawekezaji, wajasiriamali na washirika wa maendeleo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike, amesema programu hiyo itatekelezwa kupitia Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) na inalenga kufikia biashara 1,000 ndani ya kipindi cha miaka minne, ambapo kila mwaka itasaidia kampuni 250 katika sekta sita muhimu, ambazo ni madini, nishati, utalii, kilimo na ufugaji, viwanda na teknolojia.
“Tutasaidia kampuni 250 zinazomilikiwa na vijana kila mwaka kwa miaka minne, tukishirikiana kwa karibu na wizara husika ili kuhakikisha vijana wenye mawazo na makampuni yao wanapata nafasi kubwa ya kuchaguliwa, ” amesema.
Ameeleza kuwa malengo makuu ya programu hiyo ni kuharakisha ukuaji wa biashara changa zenye ubunifu na uwezo mkubwa, kugeuza matokeo ya tafiti kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti kuwa bidhaa na huduma zenye thamani ya kibiashara, kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, vyuo vikuu, sekta binafsi na wawekezaji, kuboresha upatikanaji wa mitaji na fursa za uwekezaji, pamoja na kuongeza ushindani wa kimataifa wa biashara za ubunifu za Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Amos Nungu, amesema programu hiyo ni muhimu kwani biashara nyingi changa hazina msaada maalumu wa kiufundi, matokeo ya tafiti mara nyingi hubaki maabara badala ya kufika sokoni, na wajasiriamali wachanga wanakosa mitaji na masoko.
“Mpango huu hauhusiani tu na kusaidia biashara changa bali ni juhudi za kuimarisha mfumo wa taifa wa ubunifu, ambapo serikali inatoa sera na miongozo, vyuo vikuu hutoa utafiti na utaalamu wa kitaaluma, sekta binafsi inafungua masoko, wawekezaji wanatoa mitaji na washirika wa maendeleo wanasaidia kuimarisha uwezo wa mfumo mzima wa ubunifu,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa DTBi, Patience Karua, amesema kampuni ya DTBi kwa kushirikiana na Sahara Ventures wanatarajia kutekeleza programu hiyo kwa umahiri mkubwa ili kuunda matokeo chanya katika mifumo ya biashara nchini, kusaidia vijana kuwa katika nafasi nzuri sokoni, na kuvutia wawekezaji.



