‘Samia Legal Aid’ yaleta matumaini kwa wananchi

DODOMA: PROGRAMU ya huduma ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid imeendelea kurejesha matumaini kwa wananchi baada ya kusaidia kuokoa nyumba iliyokuwa ipigwe mnada, kusuluhisha mgogoro wa shamba uliodumu kwa miaka 15 na kumaliza kesi ya mirathi iliyokaa mahakamani kwa miaka 13.
Programu hiyo ilianzishwa na Serikali takribani miaka mitatu iliyopita ikiwa na lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, ambapo hadi sasa wananchi milioni 4.1 nchini wamenufaika.
Akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na huduma hiyo, Rosemary Spendi mkazi wa Dar es Salaam alisema timu ya msaada wa kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ilimsaidia kurejeshewa nyumba yake iliyokuwa katika hatari ya kuuzwa baada ya mpangaji kukopa mkopo benki kwa nyaraka za kugushi.
“Nimehangaika na kesi hii kwa karibu miaka miwili bila mafanikio kwani haikuwahi kusikilizwa licha ya kupangiwa mahakimu watano kwa nyakati tofauti. Kupitia Samia Legal Aid mgogoro umeisha na nimerejeshwa nyumba yangu yenye thamani ya shilingi milioni 150 iliyokuwa iuzwe kwa 30m/-,” alisema huku akishauri taasisi za fedha kuchukua tahadhari kabla ya kutoa mikopo.
Kwa upande wake, Hawa Kalimeje kutoka Tunduru mkoani Mtwara alisema alikuwa na changamoto ya kesi ya mirathi iliyodumu kwa miaka 13 bila mafanikio.
“Tumezunguka mahakamani kwa muda mrefu bila suluhu, lakini baada ya kupata msaada kupitia Samia Legal Aid, shauri limepata ufumbuzi na sasa tunaelewana,” alisema.
Naye Kanduru Msusa alisema kupitia timu ya msaada wa kisheria, waliweza kuwakutanisha watoto 11 ambao walikubaliana kuuza mali za marehemu na kugawana kwa haki ndani ya kipindi cha miezi miwili.
“Tunashukuru Serikali ya Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hii kwani imerejesha hata undugu wetu. Niishauri Serikali kuendelea kuimarisha huduma hiyo hasa katika masuala ya mirathi ambayo yanachangamoto kubwa sana.”
Katika tukio lingine, Abeid Mbelengo mkazi wa Masasi mkoani Mtwara aliamua arejeshewe kiasi cha Sh 1,050,000 alichotumia kununua shamba la ekari nane mwaka 2011 ambalo liliibua mgogoro uliodumu kwa miaka 15 kati yake na mjane Flora Mkondya.
“Niliamua kuchagua amani zaidi kuliko mgogoro ambao ulikuwa unaninyima amani mimi na familia yangu, nimefanya hivyo si kwasababu sijui thamani ya shamba ambalo nimelipanda mikorosh, bali nimeamua kulirejesha ili nibaki na utulivu, amani na heshima, nirahisi mtu kuvuliwa heshima kuliko kuvikwa.”
“Nilitamani nilirejeshe hata bila senti kwa jinsi ambavyo sikutarajia kuingia kwenye mgogoro wa kesi maana nilinunua shamba katika kutoa msaada kumbe nimenunua kesi.”
Kutokana na uamuzi wake huo wa busara, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera alimkabidhi kiasi cha Sh milioni 15 kama pongezi za busara alizozionesha Mbelengo.
Akizungumza, Dk Homera alisema wizara hiyo itaendelea kuwa kimbilio la wananchi wanyonge wanaokosa haki zao na kuwataka Watanzania kuzingatia zaidi usuluhishi badala ya kukimbilia mahakamani.
“Migogoro inanyima watu amani na maendeleo, hivyo nitoe rai kwa watanzania tujikite sana kwenye usuluhishi wa migogoro na kwenda mahakamani iwe suluhisho la mwisho. Tukifanya hivi wananchi wengi watapata haki zao za msingi kwa wakati.”



