JKCI yazindua kampeni magonjwa yasiyoambukiza

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha kampeni maalumu ya “Jua Namba Zako” katika kliniki ya Kariakoo, ikiwa na lengo la kuwahamasisha wananchi kupima na kutambua mapema magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.

Kupitia kampeni hiyo, wananchi wanapata fursa ya kupima viashiria muhimu vya afya ikiwemo presha ya damu, mapigo ya moyo, kiwango cha sukari, mafuta kwenye damu, pamoja na urefu na uzito wa mwili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dk. Peter Kisenge, amesema taasisi hiyo inaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwasaidia kugundua mapema magonjwa hayo.

“Katika kuhakikisha tunawafikia wananchi walipo, leo tupo Kariakoo ambapo tunaendesha kambi ya siku tatu. Hadi sasa tumeshahudumia zaidi ya watu 226,” amesema Dk. Kisenge.

Ameeleza kuwa magonjwa ya moyo na yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi na kusababisha vifo vingi, hivyo kampeni hiyo inalenga kuyadhibiti kwa kuyagundua mapema.

Dk. Kisenge amesema katika kambi hiyo, wananchi wanapatiwa vipimo mbalimbali ikiwemo EKO na ECG, huku pia madaktari wa macho, meno, kisukari na moyo wakitoa huduma kwa pamoja.

Amefafanua kuwa kati ya watu zaidi ya 100 waliopimwa kwa kipimo cha EKO, asilimia 28 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyotokana na shinikizo la damu.

“Pia tumebaini kuwa chini ya asilimia tano ya wananchi hawakujua kabisa kuwa wana shinikizo la damu au kisukari hadi walipopimwa hapa,” ameongeza.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kujua namba zao mapema ili kurahisisha tiba na kinga.

“Ukijua presha yako, sukari yako, mafuta kwenye damu, uzito na urefu wako, inakuwa rahisi kuchukua hatua mapema kabla hali haijawa mbaya,” amesema.

Ameleza kuwa mabadiliko ya mtindo wa maisha yanaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa hayo, ikiwemo kufanya mazoezi angalau dakika 30 kwa siku, kuacha kuvuta sigara, kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi, kupunguza uzito uliozidi na kula lishe bora yenye mboga mboga na matunda kwa wingi.

Dk. Kisenge aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika kliniki ya Kariakoo ili kupata huduma hizo bure, akibainisha kuwa huduma zitaendelea kutolewa hata baada ya kumalizika kwa kambi hiyo.

“Tunawaalika wananchi wote, wakiwemo wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wanaofanya shughuli zao Kariakoo, kujitokeza kupima afya zao. Jua namba zako, okoa maisha yako,” amesisitiza Kisenge.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button