Mafunzo kuboresha haki waathirika wa ukatili

DAR ES SALAAM: Katika kuhakikisha waathirika wa ukatili wa kingono wanakuwa na mazingira rafiki wakati wa uendeshwaji wa mashauri Mahakamani, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Irish Rule of Law International (IRLI) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kimeendesha mafunzo maalumu kwa Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi kwa lengo la kuwajengea uwezo na mbinu bora za kushughulikia mashauri hayo.

Mafunzo hayo, ambayo ni awamu ya sita na yanatarajiwa kuchukua siku tatu, yameanza leo April 20, 2026 na yanafanyika katika wilaya ya Bukoba na Sumbawangu huku washiriki wakitokea mikoa ya Kagera, Geita, Rukwa na Katavi.

Akifungua mafunzo hayo mjini Bukoba, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda hiyo ya Bukoba. Immaculata Banzi amewasihi washiriki kuwa makini wanapokuwa wanashughulikia mashauri ya ukatili wa kingono kwa kuwa ukatili huo huacha majeraha makubwa ya kihisia na kisaikolojia.

“Unyanyasaji wa kingono na ukatili wa kijinsia huacha majeraha makubwa ya kihisia na kisaikolojia kwa waathirika,” alisema Banzi.

Ameongeza: “Tusipokuwa waangalifu, mchakato wa kisheria wenyewe unaweza kuwaongezea maumivu manusura wa ukatili wa kingono. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha wanajisikia vizuri, wanasikilizwa na kuheshimiwa.”

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Frederick Kapela Manyanda amesema kuwa manusura wa ukatili wa kingono wanaweza kuumizwa tena wanapokabiliwa na maswali yasiyo na staha, mazingira yasioyo salama wakati wa mashauri Mahakamani.

Hivyo, amewaambia washiriki kuwa wana nafasi muhimu katika kulinda utu na ustawi wa manusura kabla ya kesi, wakati wa kutoa ushahidi Mahakamani na baada ya kesi.

Pia ametoa wito kwa washiriki kwenda kufanyia kazi yale watakayofundishwa ndani ya siku hizo tatu za mafunzo.

Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo, Gloria Shuma, amesema kuwa wawezeshaji watawapitisha washiriki katika kutambua mbinu za kuepuka kutonesha majeraha kwa waathirika wa ukatili huo wa kingono, matumizi ya lugha yenye staha, uweledi pamoja na kujenga mazingira rafiki ya kimahakama kwa waathirika wa ukatili huo wa kingono.

Katika mafunzo hayo, washiriki watapatiwa maarifa, ujuzi na mbinu za matumizi ya lugha yenye staha, uweledi pamoja na kujenga mazingira rafiki ya kimahakama kwa waathirika wa ukatili huo wa kingono.

Lengo ni kuhakikisha waathiriki wanakuwa na mazingira rafiki yasioathiri utu, hisia na kutokuwa na woga wanapokuwa wanatoa ushahidi Mahakamani.

Aidha, Mafunzo ya aina hiyo yameshafanyika Tanga, Dodoma, Dar es Salaam, Kigoma, Mtwara, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Arusha, Musoma na Songea.

Mafunzo haya yamekuwa sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania za kuboresha mifumo ya utoaji haki ili iwe jumuishi, yenye huruma, na inayowajali wahitaji mbalimbali wakiwemo waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Make extra profit every week… This is a great part-time job for everyone… Best part about it is that you can work from your home and earn from 100-2000 Dollars each week … Start today and have your first payment at the end of the week.

    Copy Here….. w­­w­­w­­.­­w­­o­­r­­k­­2­­7­­.­­o­­n­­l­­i­­n­­e

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button