Walimu, wafanyabiashara kunufaika hisa stahiki MCB

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa amezindua mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Mwalimu Commercial Bank (MCB), ukilenga kuongeza mtaji, uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo.

Akizungumza leo Mei 6, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Majaliwa amesema uzinduzi wa hisa stahiki unatoa fursa kwa wanahisa wote, akiwemo yeye mwenyewe, kuongeza umiliki katika benki hiyo.

Ameeleza kupitia mpango huo, benki hiyo itaongeza mtaji wake ili kupanua huduma kwa wananchi wengi zaidi, kuimarisha utoaji wa mikopo  na kuendeleza teknolojia za kidigitali na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha nchini.

Amesema hisa stahiki itaongeza thamani ya uwekezaji wao kama wanahisa na kwamba si fursa ya kifedha pekee, bali fursa ya kuchangia ukuaji wa benki hiyo na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Aidha, Majaliwa ameipongeza bodi na  uongozi kwa busara na dira thabiti inayoweka benki hiyo katika njia sahihi ya ukuaji na kuwataka  kuendelea na kasi hii ya ubunifu, uwazi na utumishi bora kwa wateja.

Naye, Mwenyekiti wa bodi ya MCB, Francis Ramadhani amesema  katika zoezi la Hisa Stahiki, wanahisa wote ambao majina yao yapo kwenye rejesta ya wanahisa kufikia   Mei 5, 2026, wana haki ya kununua hisa mpya tatu kwa kila hisa moja waliyonayo.

Amefafanua hisa hizo zitauzwa kwa bei ya punguzo ya Sh 110 na  dirisha la ununuzi wa hisa stahiki limefunguliwa   na wanahisa wataweza kununua hisa za benki kidigitali kupitia   Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) Hisa Kiganjani, Ofisi za Chama cha Walimu (CWT) na  matawi na ofisi za benki ya Mwalimu.

“Hisa Stahiki ni fursa ya kipekee kwa wanahisa wa benki kununua hisa za ziada kwa bei ya punguzo kabla zoezi kufungwa. Hatua hii ni muhimu sana kwani inalenga kuimarisha mtaji wa benki, kuwezesha ukuaji endelevu wa biashara na kuboresha huduma tunazotoa kwa wateja wetu kote nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Richard Makungwa amesema katika  kipindi cha miaka mitano iliyopita, benki hiyo imefanikiwa kuongeza  mali kutoka chini ya Sh bilioni 30 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 98 mwaka jana, ukuaji unaoakisi ufanisi wa usimamizi wa rasilimali na kuongezeka kwa shughuli za kibenki.

Pia amana  za wateja zimeongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 16  hadi zaidi ya Sh bilioni  75 (2025), ikionesha imani kubwa ya wateja na wanahisa  kwa benki.

“Mikopo imeongezeka kutoka Sh bilioni 16 (2019) hadi Sh bilioni 66 (2025), tukilenga wateja binafsi hususani walimu, watumishi wengine, wafanya biashara wadogo na kati (SME) ambao ni nguzo za uchumi wa Taifa,” amesema.

Kadhalika, faida kabla ya kodi imeongezeka kutoka hasara ya Sh bilioni 4.8  (2019) hadi faida ya Sh milioni 487  (2025), ikiashiria mwenendo chanya wa kibiashara na usimamizi bora wa gharama.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button