Benki yajizatiti uchumi kidigitali

DAR ES SALAAM: BENKI ya Exim Tanzania imeendelea kujikita katika kukuza uchumi wa kidijiti kupitia matumizi ya teknolojia bunifu zinazolenga kuongeza ujumuishwaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania.

Benki hiyo imeonyesha dhamira hiyo kufuatia utambulisho wa huduma za kibenki kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp, hatua inayowawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kifedha kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijiti wa benki hiyo, Silas Matoi alisema huduma hiyo inalenga kuwapa wateja urahisi zaidi wa kupata huduma za benki kupitia jukwaa ambalo tayari linatumika na watu wengi kila siku.

Alisema huduma hiyo itawawezesha wateja kufanya miamala mbalimbali moja kwa moja kupitia WhatsApp ikiwemo kuangalia salio, kuhamisha fedha, kutuma fedha kwenda simu za mkononi, kufanya malipo kwa wafanyabiashara pamoja na kulipia huduma za serikali.

“Lengo letu ni kuhakikisha huduma za benki kidijiti zinakuwa rahisi, salama na zinazofikika kwa urahisi zaidi kwa wateja wetu,” alisema Matoi.

Aliongeza kuwa mfumo huo umejengwa kwa kuzingatia usalama wa taarifa na miamala ya wateja kupitia mifumo mbalimbali ya uthibitishaji ikiwemo matumizi ya PIN.

Aidha, alisema huduma hiyo itaongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watumiaji wengi wa WhatsApp nchini huku ikiondoa ulazima wa kupakua programu nyingine tofauti kwa ajili ya huduma za benki.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Kauthar D’Souza alisema uzinduzi wa huduma hiyo unaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya wateja.

Alisema kupeleka huduma za kifedha kupitia WhatsApp kutarahisisha matumizi ya huduma za benki kwa wananchi wengi zaidi kutokana na jukwaa hilo kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watu wengi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button