THRDC yatoa neno mauaji ya Baozhang Ge

DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umekemea vikali mauaji ya aliyekuwa mmliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI na kuitaka jamii kuacha kuhusisha matukio hayo na makabila au jamii fulani badala yake sheria ichukue mkondo wake dhidi ya wahusika wa uhalifu huo.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Kitaifa wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa amesema si sahihi jamii kuanza kujadili asili ya watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu kwani hali hiyo inaweza kuchochea chuki na migawanyiko isiyo na msingi.
 
Amesema wahalifu wanapaswa kushughulikiwa kama wahalifu wengine bila kuangalia wanatoka jamii gani huku akisisitiza kuwa jamii inapaswa kukemea mauaji ya aina zote bila kujali yametendwa na nani.
 
“Inapotokea mtu amefanya uhalifu, wahalifu hao waadhibiwe kama wahalifu wengine bila kuanza kujadili jamii walizotoka. Ninachotaka kusema ni kwamba tukemee mauaji ya aina zote bila kujali yamefanywa na nani,” amesema Wakili Olengurumwa.
 
Kauli hiyo imekuja kufuatia tukio la mauaji ya mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI Bhaozang Ge, ambapo inaelezwa aliuawa na watu wanaodaiwa ni walinzi binafsi wa kiwanda hicho kilichopo Mabibo, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumamosi ya Mei 16, 2026.
 
THRDC imeitaka jamii kushirikiana na vyombo vya dola katika kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia uchunguzi huku ikionya dhidi ya kauli zinazoweza kuleta taharuki au kuchafua jamii fulani kutokana na matendo ya watu binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button