Kamati yaipongeza TRA utendaji kazi mzuri

DAR ES SALAAM: KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Bajeti imeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utendaji kazi ambao unaiwezesha kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi waliyowekewa na Serikali kwa kila mwezi.
Akizungumza wakati wa kikao baina ya wajumbe wa Kamati hiyo na Menejimenti ya TRA Mei 30, 2026 Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mashimba Ndaki amesema TRA wanastahili pongezi kwa namna wanavyofanya kazi zao.

Aidha amewapongeza kwa kuwa na Idara maalum ya kuhudumia walipakodi wakubwa hali ambayo itawafanya walipe kodi zaidi na kuijulisha jamii kuwa hakuna anayeachwa nyuma katika masuala ya kodi na kila anayepaswa kulipa kodi analipa.
“Kumekuwa na dhana kwamba wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi, niwajulishe wananchi kuwa wafanyabiashara wakubwa nao wanalipa kodi ndiyo maana wamewekewa Idara maalumu ya kuwahudumia, na kwenye makusanyo yote ya TRA wanachangia asilimia 40,” amesema Ndaki.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde ameipongeza TRA kwa kuendelea kuongeza wigo wa kodi na kujiweka karibu zaidi na Walipakodi hali ambayo imeongeza uhiari katika kulipa kodi.
Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda ameshukuru hatua ya Kamati ya Bunge kuzitembelea ofisi za Idara ya Walipakodi Wakubwa na kueleza kuwa ziara hiyo itazidi kuwahamasisha Walipakodi hao kuendelea kulipa kodi.

Amesema TRA itaendelea kutenda haki kwa Walipakodi wote kwa kuzingatia madaraja yao kwa yule anayestahili kulipa kikubwa atalipa kikubwa, anayestahili kulipa kidogo atalipa kidogo na yule asiyestahili kulipa hatolipa kwa kuwa huo ndiyo utaratibu wa utendaji wa Mamlaka hiyo.



