Wabunifu watakiwa kusajili bunifu zao

ARUSHA: Uwekezaji katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kwa vijana ni hatua muhimu ya kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kimataifa na kuchangia uchumi wa ajira kupitia miradi ya kibunifu.

Lakini pia bunifu zote zinazozalishwa na wanafunzi shuleni zinapaswa kusajiliwa ili kulinda haki za wabunifu ili kuzuia teknolojia hizo kuibwa au kutumiwa na watu wengine bila idhini.

Akizungumza katika maonesho ya bunifu yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Arusha Science Mkoani Arusha, Profesa ,Thomas Kivevele ambaye ni Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST)amesema bunifu zinazozalishwa shuleni hapo zina mchango mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, pamoja na kufungua fursa za ajira kwa vijana.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Arusha Science, Profesa Nuhu Hatibu, amewataka wazazi na walezi kuwajengea watoto mazingira bora ya kukuza vipaji vya ubunifu tangu wakiwa wadogo ili waweze kuonyesha umahiri wao na kujipatia ajira.

“Wanafunzi wanapoanzisha kampuni kupitia bunifu zao, ni muhimu waendelee kushirikiana hata wanapojiunga na elimu ya juu, ushirikiano huo utawasaidia kuendeleza kampuni zao na kuzalisha ajira kwa wengine,”

Profesa, Hatibu amesisitiza kuwa ujuzi na umahiri katika teknolojia, hususan kupitia mkondo wa amali, ni muhimu katika kuendeleza ubunifu na kuongeza kuwa uchumi wa dunia unabadilika kwa kasi, hivyo uvumbuzi wa kisayansi unapaswa kugeuzwa kuwa teknolojia zinazotoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wananchi.

Awali Mkuu wa Kitengo cha Sayansi shuleni hapo, Ally Msangi amesema wanafunzi hao wamefundishwa kujiamini, kutatua changamoto za kijamii na kuongeza umahiri wa kujieleza mbele ya hadhira.

“Maonesho haya yanawapa wanafunzi fursa ya kuwasilisha mawazo yao kwa kujiamini, kuonyesha vipaji vyao na bunifu mbalimbali zinazodhihirisha uwezo wao wa kipekee katika nyanja tofauti”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button