Kiswahili hazina ya Tanzania

WAKATI mataifa mengi duniani yakitafuta njia za kukuza uchumi, kuimarisha diplomasia na kuunganisha wananchi wake, Tanzania inaendelea kunufaika na hazina kubwa ya lugha ya Kiswahili ambayo sasa imekuwa alama ya utambulisho wa Afrika na daraja la mawasiliano ya kimataifa.
Kutoka Marekani hadi China, Ujerumani hadi Korea Kusini, Kiswahili kinaendelea kufundishwa katika taasisi mbalimbali za elimu huku mahitaji ya wataalamu wa lugha hiyo yakiongezeka siku hadi siku.Ukuaji wa lugha ya Kiswahili pia umefungua fursa mpya za ajira, biashara, teknolojia na uwekezaji kwa Watanzania.
Katika mahojiano maalumu na Daily News Digital yaliyofanyika katika ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), wataalamu wa lugha hiyo wameeleza namna Kiswahili kilivyotoka kuwa lugha ya mawasiliano ya kawaida hadi kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na diplomasia duniani.SOMA:Jifunze Kiswahili
Mchunguzi Lugha Mwandamizi wa BAKITA, Ambrose Mghanga, amesema asili ya Kiswahili inatokana na lugha za Kibantu zilizokuwa zikizungumzwa katika mwambao wa Afrika Mashariki kabla ya ujio wa wageni.Amesema lahaja mbalimbali zikiwemo Kiunguja, Kipemba, Kilamu na Kingazija zilikuwa zikitumika katika biashara na mawasiliano kati ya jamii za pwani na kuchangia kukua kwa lugha hiyo.
“Watu wa pwani walikuwa wanafanya biashara na kuwasiliana kwa kutumia lugha zilizofanana. Taratibu Kiswahili kikawa lugha iliyowaweka pamoja,” amesema Mghanga. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ujio wa Waarabu, Wajerumani na Waingereza uliisaidia lugha hiyo kuenea zaidi kutokana na matumizi yake katika biashara, elimu na shughuli za utawala.
Hata hivyo, hatua kubwa zaidi katika maendeleo ya Kiswahili ilikuja baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 wakati Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipoipa lugha hiyo nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa. Mghanga amesema uamuzi wa kuitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa uliimarisha umoja wa Watanzania na kuwezesha wananchi kutoka makabila mbalimbali kuwasiliana kwa urahisi.

Aidha, mwaka 1967 Serikali ilianzisha Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili kusimamia maendeleo ya lugha hiyo, huku mwaka uliofuata Kiswahili kikianza kutumika kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi. “Ndiyo maana leo ukienda sehemu nyingi nchini hakuna haja ya mkalimani. Kiswahili kimechangia kwa kiasi kikubwa kudumisha umoja na amani ya nchi,” amesema.
Kadri miaka ilivyopita, Kiswahili kimeendelea kuvuka mipaka ya Tanzania na Afrika Mashariki na kupata nafasi kubwa katika mataifa mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa BAKITA, zaidi ya vyuo 100 nchini Marekani vinafundisha Kiswahili, huku nchi nyingi zikiendelea kufungua madarasa maalumu kwa ajili ya kujifunza lugha hiyo.
Ukuaji huo umekifanya Kiswahili kuwa chanzo kipya cha fursa za kiuchumi kwa vijana wa Kitanzania. Msanifu Lugha wa BAKITA, Kusanja Emmanuel, amesema maeneo kama ukalimani, tafsiri, ufundishaji wa Kiswahili, uandishi wa vitabu, utengenezaji wa maudhui ya kidijitali na utalii yanaendelea kutoa ajira kupitia matumizi ya lugha hiyo.
“Zamani watu walikuwa wanaona Kiswahili kama lugha ya kawaida tu, lakini sasa kinaweza kuwa bidhaa inayokuingizia kipato,” amesema. Mbali na uchumi, Kiswahili kinaendelea kupata nafasi kubwa katika maendeleo ya teknolojia za kisasa. Mchunguzi Lugha Mkuu wa BAKITA, Fatma Mlaki, amesema taasisi hiyo imeanza kuandaa hifadhidata kubwa ya Kiswahili kwa ajili ya matumizi ya teknolojia mbalimbali ikiwemo Akili Bandia (AI).
Amesema hadi sasa zaidi ya maneno milioni 61 yamekusanywa kwa lengo la kusaidia maendeleo ya mifumo ya kidijitali inayotumia lugha ya Kiswahili. “Tunataka kuhakikisha Kiswahili hakiwi nyuma katika mapinduzi ya teknolojia yanayoendelea duniani,” amesema. Katika eneo la diplomasia, Kiswahili kimeendelea kupata mafanikio makubwa katika majukwaa ya kimataifa.
Mlaki amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, huku Umoja wa Afrika ukiitambua Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika katika shughuli zake. Kwa Tanzania, mafanikio hayo yanaonyesha kuwa Kiswahili sasa si tu lugha ya mawasiliano, bali pia ni sauti ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa.
Kutokana na ukuaji huo, Tanzania inatarajia kufanya Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili jijini Paris, Ufaransa mwaka 2026, likiwa na lengo la kuitangaza lugha hiyo pamoja na kufungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji. Wataalamu wa lugha hiyo wanasema wakati umefika kwa vijana kuitumia Kiswahili kama nyenzo ya kujenga ajira, kuendeleza ubunifu na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi duniani.
Katika dunia inayobadilika kwa haraka, Kiswahili hakibaki tena kuwa lugha ya mazungumzo ya kawaida pekee, bali limekuwa rasilimali muhimu ya maendeleo na urithi ambao Tanzania inaendelea kuutangaza duniani.



