Mradi wa ‘Wezesha Wasichana’ awamu ya pili wazinduliwa

MAFIA: Awamu ya Pili ya mradi wa “Wezesha Wasichana  Tabasamu Mpaka Mwisho” uliofadhiliwa na  C-Weed Mwani, CEAMSA na  Cargill, uliozinduliwa na Shirika la Harakati na Uwezeshaji wa Mazingira Tanzania  (TEEMO) unalenga kuwawezesha wasichana wa shule za sekondari kupitia elimu ya afya.

Elimu hiyo ni ya hedhi, usafi binafsi, utunzaji wa mazingira, kujenga kujiamini, kuboresha ufaulu wa masomo pamoja na upatikanaji wa taulo mbadala za kike (Reusable Pads).

Mradi huo unalenga kuboresha usimamizi wa afya ya hedhi kwa wasichana, kupunguza utoro shuleni unaotokana na changamoto za hedhi, kuimarisha usafi binafsi, kuongeza ufaulu wa masomo, kujenga kujiamini na uwezo wa uongozi kwa wasichana, pamoja na kuhamasisha matumizi ya bidhaa rafiki kwa mazingira kupitia taulo mbadala za kike.

Akizindua mradi huo, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Taifa Costantino amewashukuru wadau hao kwa hatua muhimu ya kumsaidia mtoto wa kike na kuwasisitiza wanafunzi kuhakikisha wanaendeleza tamaduni ya usafi na kutunza mazingira.

Aidha, ametoa wito kwa wanafunzi hao kuwatumia vizuri walimu wao wa malezi pindi wanapopata changamoto zao wawapo shuleni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TEEMO, Winfrida Shonde, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa wasichana kama njia ya kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.

“Tunaamini kuwa msichana mwenye afya bora, elimu bora, kujiamini na mazingira salama ana nafasi kubwa zaidi ya kufikia ndoto zake na kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania.” alieleza

Mradi huo umejengwa katika nguzo sita muhimu ambazo ni patikanaji wa taulo mbadala za kike (Reusable Pads), elimu ya afya ya hedhi na usafi binafsi, kujenga kujiamini na kukuza uongozi kwa wasichana, kuboresha mahudhurio shuleni na ufaulu wa masomo, kukuza mazingira ya shule yasiyo na unyanyasaji wala vitendo vya kudhalilisha wanafunzi pamoja na kupunguza matumizi ya plastiki na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button