Mafanikio ya mradi wa Pamba na Kazi Bora yaonekana

DAR ES SALAAM: MRADI wa Pamba na Kazi Bora unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali za Tanzania na Brazil umeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya ajira za watoto, huku ukichangia kuimarisha usalama na afya kazini na kupanua huduma za ulinzi wa kijamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam ,Ofisa Programu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Noreen Toroka wakati wa mkutano wa siku tatu kujadili namna ya kupambana na utumikishwaji wa watoto kwenye kilimo cha pamba kupitia mradi wa Cotton with Decent Work unaoratibiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026 ukiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa taasisi za umma, vyama vya wafanyakazi na waajiri katika kubuni na kutekeleza sera zinazolenga kutokomeza ajira ya watoto katika sekta ya pamba.
Alisema mradi huo umejikita katika kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa kazi, kukuza usalama na afya kazini (OSH) na kuongeza upatikanaji wa huduma za ulinzi wa kijamii kama njia ya kuzuia watoto kuingia katika shughuli za kazi zinazohatarisha ustawi wao.
Toroka alisema wilaya ya Meatu mkoani Simiyu ni mkoa uliochaguliwa kuwa eneo kuu la utekelezaji kutokana na mchango wake mkubwa katika uzalishaji wa pamba nchini. ”Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka wa kilimo wa 2021/2022, Mkoa wa Simiyu ulichangia takribani asilimia 61 ya uzalishaji wote wa pamba nchini, huku Meatu ikiwa miongoni mwa wilaya zenye uzalishaji mkubwa lakini zinazokabiliwa na changamoto ya ajira ya watoto.
”Katika kipindi cha utekelezaji wa mradi, maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu (PMO-LER) pamoja na OSHA walishiriki programu za kubadilishana uzoefu nchini Brazil sambamba na washiriki kutoka Belize, Suriname, Colombia, Ethiopia, Peru na Uganda,”alisema
Alisema mafunzo hayo yalijikita katika masuala ya ajira ya watoto, ukaguzi wa kazi, usalama na afya kazini pamoja na haki za msingi kazini,maarifa yaliyopatikana kupitia ushirikiano huo yamechangia kuboresha utekelezaji wa shughuli mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo mafunzo kwa wakaguzi wa kazi, tafiti za ulinzi wa kijamii, huduma za msaada wa kisaikolojia na kuimarisha usalama katika mlolongo wa thamani wa pamba.
Aidha, alisema mradi huo pia umefanikiwa kuendesha ukaguzi maalum wa kazi katika maeneo yanayozalisha pamba wakati wa misimu ya uvunaji ya mwaka 2024 na 2025. Ukaguzi huo ulianza katika Wilaya ya Meatu kabla ya kupanuliwa katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
”Kupitia ukaguzi huo, AMCOS 30 pamoja na viwanda vinne vya kusindika pamba vilifikwa na mafunzo kuhusu madhara ya ajira ya watoto, wajibu wa waajiri, pamoja na umuhimu wa usalama na afya kazini huku wakulima na viongozi wa vyama vya ushirika nao walipewa elimu kuhusu namna ya kuwalinda watoto dhidi ya kazi hatarishi na kuzingatia mazingira salama ya kazi.
Kwa upande wake Kiongozi wa Programu ya Ushirikiano wa Kusini-Kusini wa ILO kutoka Brazil, Fernanda Barreto, alisema Tanzania na Brazil zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika kupambana na ajira za watoto na kuboresha mifumo ya usalama wa kijamii kupitia mradi wa pamoja unaoratibiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Alisema mradi huo umewezesha pande zote mbili kujadiliana kwa kina kuhusu changamoto za ajira za watoto pamoja na njia za kuimarisha ulinzi wa kijamii kwa wananchi wanaofanya kazi katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Barreto alisema kupitia utekelezaji wa mradi huo, Tanzania imepiga hatua muhimu ikiwemo kuandaa mkakati wa kitaifa wa kuondoa ajira za watoto na kutekeleza kampeni mbalimbali za uhamasishaji kwa jamii zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu madhara ya tatizo hilo.
“Tumekuwa hapa Tanzania kwa wiki moja kujadili masuala ya ajira za watoto na usalama wa kijamii. Tumefurahishwa na maendeleo yaliyopatikana, hususan katika maandalizi ya mkakati wa kitaifa wa kuondoa ajira za watoto pamoja na kampeni za uhamasishaji zilizofanyika katika maeneo mbalimbali,” alisema Barreto.
Alisema kuwa pamoja na juhudi hizo, mradi huo umefungua jukwaa la majadiliano kati ya Tanzania na Brazil kuhusu namna ya kuendeleza mifumo ya usalama wa kijamii inayoweza kuwafikia wakulima na wafanyakazi wa sekta ya kilimo ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii.
Alisema tathmini ya utekelezaji wa mradi huo inaonesha kuwa malengo mengi yaliyowekwa mwanzoni yamefikiwa kwa mafanikio, jambo lililoifanya Serikali ya Tanzania kuonesha nia ya kuona ushirikiano huo ukiendelea kwa awamu nyingine.
“Tumepokea maombi kutoka Serikali ya Tanzania ya kuendeleza zaidi mradi huu. Serikali ya Brazil itafanya mashauriano kuona namna bora ya kuendeleza shughuli hizi kupitia ushirikiano wa pande tatu unaohusisha Brazil, ILO Tanzania na wizara za kazi za nchi zote mbili,”alisema.



