Mpogolo: Huna uwezo usiombe kazi

DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wakandarasi wenye nia ya kwenda kuomba kazi katika wilaya hiyo kuhakikisha wana uwezo wa kufanya kazi hizo na kutimiza wajibu wao kikamilifu.
 
Mpogolo ametoa angalizo hilo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kimanga-Mazda yenye urefu wa mita 400 iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.7 fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.
 
Akizungumza baada ya kukagua barabara hiyo Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga kiasi cha Sh bilioni 14 kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kutengeneza na kuboresha barabara ndani ya Jiji hilo hali ambayo itafanya wakandarasi wengi kuvutiwa kuja kuomba mkataba wa kufanya kazi za ujenzi wa barabara.
 
“Najua kwa kiasi hiki cha fedha wakandarasi wengi watatamani kuja kuomba kazi hapa kwetu Ilala, ila hatutawavumilia wakandarasi wasiokuwa na uwezo, kama huna uwezo usije kuomba kazi hapa,” amesisitiza Mpogolo.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha katika miradi mbalimbali ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Barabara hiyo inayojengwa na mkandarasi mzawa kampuni ya Osaka Construction Ltd imetajwa kuwa ni kiungo muhimu kati ya Wilaya ya Ilala na Ubungo ambayo hapo awali ilikuwa na changamoto ya kupitika hasa nyakati za mvua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button