Bunge latoa neno kukwama kwa miradi PPP

DODOMA: Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeingilia kati kusuasua kwa miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), likionya kuwa kukwama kwa miradi hiyo kunasababisha hasara kubwa ya mapato ya taifa na kuchelewesha ahadi za maendeleo kwa wananchi.
Kufuatia hali hiyo Juni 15, 2026, Spika wa Bunge ametoa agizo hilo na la haraka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha PPP, David Kafulila, kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, kuhakikisha wanawasilisha orodha na mchanganuo kamili wa miradi yote nchini katika kikao pamoja na kamati ya bajeti bungeni tarehe 25, June 2026.
Aidha Spika ameonyesha kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakiondoka nchini au kujitoa kwenye miradi kutokana na kuwepo kwa mazingira ya kisheria yasiyotabirika au sheria zinazotajwa kuwa “kandamizi.” Bunge limetaka kufanyika kwa marekebisho ya sheria na mifumo ili kuvutia na kuwahifadhi wawekezaji hao wa sekta binafsi.
Spika amebaisha mwisho wa taarifa yake bungeni kuwa miradi ya PPP ikipitishwa na kusimamiwa kisheria, itazalisha fedha na mapato ambayo Serikali itayatumia moja kwa moja kuboresha huduma za msingi za jamii, zikiwemo ujenzi wa makazi bora ya wananchi, uboreshaji wa mishahara ya watumishi wa umma na Kuimarisha sekta za afya na elimu nchini.



