BMH yahimiza Watanzania kuchangia mfuko wa upandikizaji figo na uloto
DODOMA: HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) imeendelea kuwataka Watanzania kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji upandikizaji wa figo na uloto kwa kuchangia Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto, huku ikieleza kuwa mafanikio ya huduma hizo yameifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba barani Afrika.
Akizungumza wakati wa ziara ya wajumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) waliotembelea hospitali hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk Abdallah Baja matibabu kwa magonjwa hayo ni kubwa hivyo kuwa kikwazo kwa wagonjwa wengi wasiokuwa na uwezo wa kumudu huduma hizo muhimu.
Alisema katika kuelekeza kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa BMH, imeanzisha Mfuko ambao umelenga kusaidia matibabu wagonjwa 100 wa kupandikizwa figo na uloto ambao wako kwenye foleni ya matibabu.
Alisema michango inapokelewa kupitia Control Number 986930000001 yenye jina la akaunti BMH ORGAN TRANSPLANT, akisisitiza kuwa mshikamano wa Watanzania unaweza kuokoa maisha ya wagonjwa wengi.
“Gharama za upandikizaji wa figo zinaanzia shilingi milioni 45 huku upandikizaji wa uloto ukigharimu takribani Sh milioni 75 kwa mgonjwa mmoja. Tunahitaji Watanzania tushirikiane kuhakikisha wagonjwa wasiokuwa na uwezo wanapata huduma hizi.”
Alisema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote pia unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa kupanua uwezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kugharamia matibabu ya gharama kubwa.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliipongeza BMH kwa mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na kutoa wito kwa Watanzania kuunga mkono mfuko wa upandikizaji ili wagonjwa wengi zaidi wanufaike.
“Tuwapongeze BMH kwa mafanikio makubwa ya utoaji huduma za afya za ubingwa na ubingwa bobezi, hususan huduma ya upandikizaji wa uloto na figo na mmeonesha uwezo mkubwa wa kitaalamu.”
Alisema mazingira na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ni za kiwango cha juu, jambo linalowafanya wagonjwa kuanza kupata nafuu hata kabla ya kuonana na daktari kutokana na mapokezi na huduma bora wanazopata.
“Nitoe wito kwa Watanzania kuendelea kuchangia matibabu ya wagonjwa wa selimundu na figo kupitia mifumo iliyowekwa, akisisitiza kuwa mchango wa kila mwananchi una umuhimu mkubwa katika kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hizo.”
Naye Meneja wa NHIF Mkoa wa Dodoma, Irene Kataraihya, alisema uchangiaji huo unalenga kuokoa maisha ya watanzania wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu na kuwahimiza wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ili kupata unafuu wa kugharamia matibabu.
“Matibabu ni gharama ndio maana bima ya afya haikwepeki, kwa wagonjwa haya mfuko unasaidia kulipia vipimo dawa na huduma za matibabu baada ya upasuaji.
Alisema Serikali tayari imetenga Sh bilioni 48 kwa mwaka kugharamia kaya zisizo na uwezo zilizotambuliwa awamu ya kwanza ya utambuzi huku akisisitiza kuwa bima ya afya ni nyenzo muhimu ya kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.
Naye Daktari Katika hatua nyingine, BMH imeandika historia baada ya kufanikiwa kuponyesha watoto 30 waliokuwa na ugonjwa wa selimundu kupitia huduma ya kisasa ya upandikizaji wa uloto.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dk Happiness Igogo, alisema BMH imeponyesha watoto 30 waliokuwa na ugonjwa wa selimundu kupitia huduma ya kisasa ya upandikizaji uloto na kwa sasa wanatarajia kumpandikizia uloto mtoto wa 31 huku wakiajiandaa kuanza matibabu kwa mtoto wa 32.
Daktari Bingwa wa Kitengo cha Figo, Dk Ayub Mashambo alisema BMH pimepandikiza figo kwa wagonjwa 56 na kati ya hao wagonjwa watatu ni kutoka nje ya nchi, jambo linaloifanya Tanzania kuendelea kujijengea sifa kama kitovu cha utalii tiba.
BMH ilianzishwa mwaka 2015 na kwa sasa ina uwezo wa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,200 kwa siku huku likiwa na huduma 20 za ubingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi ikiwamo upandikizaji wa uume ambapa wanaume 14 tayari wamehudumiwa kwa gharama ya Sh milioni 10 kwa kila mgonjwa.



