Yas, FTCC waanzisha mafunzo ya kidijitali kwa wajasiriamali

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya huduma za kidijitali na mawasiliano ya Yas, kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara wa Ufaransa Tanzania (French Tanzania Chamber of Commerce), imeanzisha programu maalumu ya mafunzo kwa wajasiriamali na watu wanaotarajia kuanzisha biashara, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kuendesha biashara zao kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mauzo wa Yas Business anayeshughulikia wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs), Gabriel Ndobho, amesema mafunzo hayo yataendeshwa kwa kipindi cha miezi sita na yatawalenga kuwapatia washiriki ujuzi muhimu wa uendeshaji wa biashara.

Amesema washiriki watafundishwa masuala mbalimbali ikiwemo usimamizi wa fedha, namna ya kufanya matangazo ya biashara, kutafuta na kuwafikia wateja pamoja na kutumia teknolojia katika kukuza biashara zao.

“Tumeamua kuwalenga wajasiriamali kwa sababu kundi hili lina mchango mkubwa katika uchumi. Tanzania ina zaidi ya wajasiriamali milioni tatu ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa pato la taifa. Kupitia mpango huu tunaleta suluhisho litakalowasaidia kuingia kwenye mfumo wa kidijitali, kwa kuwa bado wengi wanaendesha biashara zao kwa kutumia njia za kizamani,” amesema Ndobho.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka kampuni ya Charge Africa Ltd na mshiriki wa mafunzo hayo, Tony Mlella, amesema programu hiyo itawasaidia wafanyabiashara kubadili namna wanavyoendesha shughuli zao kwa kuhamia kwenye mifumo ya kisasa ya kidijitali.

Amesema pia mafunzo hayo yamekuwa fursa ya kuwajengea wafanyabiashara mtandao wa kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kukuza biashara.

Naye mshiriki Gloria Muro amesema miongoni mwa mambo aliyojifunza ni umuhimu wa kuanza biashara mara baada ya kupata wazo zuri na mtaji unaohitajika, badala ya kusubiri hadi kupata fedha nyingi.

Ameongeza kuwa ni muhimu kufanya utafiti wa soko kabla ya kuanzisha biashara, kutambua tofauti ambayo biashara hiyo italeta pamoja na kujua washirika muhimu wa kushirikiana nao ili kuongeza nafasi ya mafanikio.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button