Tanzania, Indonesia zadhamiria kushirikiana kibiashara

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Indonesia unaleta matokeo chanya kwa kuongeza thamani ya biashara, uwekezaji na matumizi ya teknolojia kati ya nchi hizo mbili.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Prof. Ulingeta Mbamba, wakati akizungumza katika hafla ya Siku ya Indonesia iliyofanyika kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Prof. Mbamba amesema Indonesia imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo maendeleo ya viwanda, usindikaji wa mazao ya uvuvi, teknolojia za kilimo cha majini, uzalishaji wa mavazi, bidhaa za matumizi ya kila siku, nishati pamoja na maendeleo ya viwanda kwa ujumla.
Aidha, amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta za madini, utalii, uchumi wa buluu, viwanda na maendeleo ya miundombinu, hali inayoweka msingi imara wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
“Serikali, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, ina dhamira ya kuhakikisha ushirikiano huu unazaa matokeo chanya kwa kuongeza thamani ya biashara kati ya nchi zetu, kuhamasisha ubia katika uwekezaji, kuimarisha matumizi ya teknolojia na maarifa, pamoja na kusaidia ushirikiano wa kibiashara kati ya kampuni za Tanzania na Indonesia,” amesema Prof. Mbamba.

Ameongeza kuwa Serikali inatarajia kuona kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Indonesia kikiendelea kukua kwa uwiano, ambapo bidhaa nyingi zaidi kutoka Indonesia zitapata soko nchini Tanzania na bidhaa za Tanzania zitaingia kwa wingi zaidi katika soko la Indonesia.
Kwa mujibu wa Prof. Mbamba, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na TanTrade imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa kuendeleza maendeleo ya viwanda, kuhamasisha uongezaji thamani wa bidhaa, kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kujenga mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa biashara.
Akizungumzia Maonesho ya Sabasaba, amesema yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji, huku yakichangia kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na washirika mbalimbali wa maendeleo.
Pia amepongeza Indonesia kwa kushiriki maonesho hayo kwa miaka mitatu mfululizo, akisema hatua hiyo inaonesha imani kubwa waliyonayo katika maonesho hayo pamoja na dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano wa biashara na uchumi na Tanzania.
Kwa upande wake, Naibu Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Priadji Soelaiman, amesema Tanzania na Indonesia zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia, ambao umeendelea kuzaa matunda katika kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi wa nchi hizo mbili.




