Kafulila azungumzia mchakato ujenzi barabara Tunduma – Igawa

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre), David Kafulila, amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara ya Tunduma–Igawa–Mbeya kupitia mfumo wa PPP.
Amesem hatua hiyo itaboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza ufanisi wa kiuchumi.
Kafulila amesema kwa sasa upembuzi yakinifu (feasibility study) unaendelea kufanywa na kampuni ya CCECC kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya haraka (expressway) kutoka Igawa hadi Tunduma.
Mradi huo unaolenga kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi katika mpaka wa Tunduma, ambayo inabeba zaidi ya asilimia 70 ya mizigo inayotoka katika Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi jirani
Ameeleza kuwa kuna hasara kubwa ya kiuchumi inayotokana na upungufu wa ufanisi wa miundombinu ya barabara, hali inayoweza kusababisha baadhi ya wafanyabiashara kuhamisha njia za usafirishaji, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuharakisha maboresho ya miundombinu hiyo ili kulinda ushindani wa ushoroba wa Tanzania katika biashara ya kikanda.
Ameongeza kwa kusema kuwa, kwa sasa Tanzania inahitaji takribani Sh trilioni 2 kila mwaka kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara zilizopo jambo linaloonyesha mzigo mkubwa wa kifedha kwa Serikali endapo itaendelea kutegemea bajeti ya umma pekee, hivyo kuhitaji ubia na sekta binafsi katika baadhi ya maeneo yenye ufanisi wa kiuchumi.



