Miradi ya BRAC yabadili maisha ya wananchi Iringa
Miradi ya BRAC yabadili maisha ya wananchi Iringa, Dk Gwajima apongeza

IRINGA: Mabadiliko ya maisha ya wanawake, wasichana na watoto mkoani Iringa yameendelea kushika kasi kupitia programu za uwezeshaji zinazolenga kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii, huku Serikali ikieleza kuwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ni msingi muhimu wa kufikia jamii yenye uwezo wa kujitegemea.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, wakati wa ziara yake mjini Iringa ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania.
Katika ziara hiyo, Waziri Gwajima alitembelea vikundi vya wanawake vinavyofanya shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo, pamoja na vituo vya malezi ya awali ya watoto vinavyolenga kuboresha makuzi ya watoto na kuwawezesha wazazi, hususan wanawake, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
Dk Gwajima alisema Serikali imeridhishwa na mchango wa BRAC katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuwawezesha wanawake, wasichana na makundi maalum, akieleza kuwa programu hizo zinaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga jamii yenye watu wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

Alisema kutokana na ukubwa wa nchi na idadi ya wananchi, Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake, hivyo ushirikiano na wadau wa maendeleo wanaotekeleza miradi yenye matokeo chanya ni muhimu katika kuharakisha maendeleo.
“Nchi ni kubwa na wananchi ni wengi. Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu. Ushirikiano na wadau wa maendeleo kama BRAC ni muhimu katika kufikia wananchi wengi zaidi,” alisema.
Waziri Gwajima aliwataka wanawake wanaonufaika na miradi hiyo kutumia fursa wanazopata kama hatua ya kujenga msingi wa kujitegemea kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa uaminifu, mshikamano na uongozi bora ndani ya vikundi.
Alisema vikundi hivyo vinapaswa kuwa daraja la kuwasaidia wanawake kutoka hatua ya kuunganisha nguvu hadi kufikia uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara zao binafsi.

“Kuunda na kuendesha vikundi si jambo rahisi. Kunahitaji uongozi makini, mshikamano na mafunzo endelevu ili viwe imara na kutimiza malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
Aidha, alimwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu, ushauri na ufuatiliaji kwa wanufaika wa miradi hiyo ili kuhakikisha wanatumia vizuri fursa walizopata na kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa BRAC Maendeleo Tanzania, Nasikiwa Duke Mwalisu, alisema kupitia programu ya Accelerating Impact for Young Women (AIM), taasisi hiyo inalenga kuwafikia wasichana na wanawake 725,252 wenye umri wa miaka 12 hadi 35 ndani ya kipindi cha miaka 10.
Alisema programu hiyo iliyoanza mwaka 2023 inalenga kutoa mafunzo ya ujuzi, stadi za maisha, msaada wa kifedha, vifaa na mitaji kwa wanawake na wasichana ili kuwawezesha kuanzisha au kukuza shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Mwalisu, asilimia 35 ya wanufaika watapatiwa msaada wa kifedha utakaowawezesha kuendelea au kurejea shuleni, huku asilimia 65 wakipata mafunzo na nyenzo za kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato.
Alisema BRAC pia inalenga kushirikiana na shule 400 kuboresha mazingira ya kujifunzia, kuanzisha vikundi vya kijamii zaidi ya 13,000 pamoja na vituo 300 vya malezi ya awali ya watoto nchini.
Kwa Mkoa wa Iringa, Mwalisu alisema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi mwaka 2023, BRAC imewafikia zaidi ya washiriki 17,000 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.
Alisema taasisi hiyo pia imeanzisha vituo 10 vya malezi ya awali ya watoto vilivyohudumia watoto 165, huku vikundi mbalimbali vikiendelea kujihusisha na kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine za kuongeza kipato.
Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Iringa (NaCoNGO), Fidelis Emilio Filipatari, alisema mashirika yasiyo ya kiserikali yameendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kufikisha huduma za maendeleo kwa wananchi.
Alisema Mkoa wa Iringa una mashirika 431 yaliyosajiliwa na yanayotekeleza miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, watoto, uchumi na maendeleo ya jamii.
Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa mashirika hayo kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa endelevu ili wananchi waendelee kunufaika hata baada ya kipindi cha ufadhili kumalizika.
Wanufaika wa miradi ya BRAC Maendeleo Tanzania wanasema programu hizo zimewasaidia kuongeza kipato na kujenga uwezo wa kujitegemea kupitia mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha, kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo.
Mbali na uwezeshaji wa kiuchumi, wamesema miradi hiyo imechangia kuboresha ustawi wa watoto na jamii baada ya kuanzishwa kwa vituo vya malezi ya awali vinavyowapa watoto mazingira bora ya ukuaji na kujifunza, huku wazazi wakipata muda wa kushiriki shughuli za uzalishaji mali.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alisema halmashauri hiyo imeendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kutekeleza programu ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.
Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, zaidi ya Sh milioni 400 zimetolewa kwa makundi hayo, huku zaidi ya Sh bilioni 1.2 zikiwa tayari zimetolewa tangu kuanza kwa mpango huo.
Alisema baadhi ya wanufaika wamewezeshwa kupata vitendea kazi kama pikipiki na bajaji ili kuongeza uwezo wao wa kuzalisha kipato na kuboresha maisha yao.



