Serikali yataka andiko umri wa kustaafu wahadhiri

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza jumuiya ya vyuo vikuu nchini kukaa pamoja kujadili umri wa kustaafu kwa wahadhiri kisha waandike andiko na kulipeleka kwake kwa uamuzi.
Alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake aliyoifanya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dar es Salaam jana kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo hicho.
Alitoa agizo hilo baada ya Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda kumwomba kuwa serikali iongeze umri wa kustaafu kwa wanataaluma wenye Shahada ya Uzamivu uanzie miaka 60 mpaka 70.
“Hili linahusu wote elimu ya juu, serikali iongeze umri wa kustaafu wana taaluma wenye PhD hadi miaka 70,” alisema Profesa Bisanda.
Profesa Bisanda alisema wamekuwa wakiona maprofesa wanapostaafu vyuo vya umma na miaka 60 wanaenda vyuo binafsi na kuboresha mazingira ya vyuo hivyo.
Dk Mpango alisema duniani kote rasilimali muhimu ni kuwekeza kwenye elimu.
“Kama hujawekeza kwenye ubora wa rasilimali watu taifa lolote litachelewa,” alisema.
Alisema serikali itaendelea kuboresha chuo hicho na mazingira yake ili kutoa elimu iliyo bora kwa kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.
Akizungumzia deni la majengo ya sekondari ya Biafra la Sh bilioni 1.6 ambayo chuo hicho kimekuwa kikiyatumia, Dk Mpango alimwagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuhakikisha linalipwa.
“Ninakuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Mkenda, kutoa kipaumbele cha juu kukamilisha malipo ya jengo la Biafra.
“Ninataka ushirikiane na Waziri wa Fedha, wadau wa maendeleo ikiwepo Benki ya Dunia kukamilisha hili jambo ikiwa ni pamoja na kukarabati majengo ya chuo hiki. Kwa hili na mimi nitatumia ofisi yangu nitawasaidia,” alisema Dk Mpango.
Kwenye changamoto ya kupata ardhi ya kujenga Makao Makuu Dodoma, alimtaka Profesa Mkenda kuzungumza na Mkurugenzi wa Jiji Dodoma ili akiwezeshe chuo hicho kipate ardhi ya kutosha.
Kuhusu gharama kubwa za intaneti, alimtaka Profesa Mkenda kuzungumza na kampuni za simu ili kutoa vifurushi rafiki kwa chuo hicho.
Awali Profesa Bisanda alisema chuo hicho kina vituo nchi nzima, kina vituo vya mitihani 66 kati ya hivyo 36 viko katika baadhi ya wilaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Mizengo Pinda alisema mchango wa OUT ni mkubwa kwa kuwa watumishi wengi serikalini wamenufaika na elimu inayotolewa na chuo hicho.
Naye Profesa Mkenda akimkaribisha Dk Mpango alisema msukumo wa serikali ni kuongeza udahili hivyo kwa chuo hicho kina nafasi kubwa.
Alisema serikali itaendelea kusaidia chuo hicho chenye matawi nchi nzima.



