Soka la Tanzania litajengwa watanzania

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema ukosoaji wenye nia njema ni sehemu muhimu ya maendeleo ya soka nchini kwa kuwa husaidia kubaini changamoto na kuimarisha utendaji wa shirikisho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,Karia amesema TFF inathamini maoni ya wadau na itaendelea kuyapokea ili kuboresha maendeleo ya mchezo huo. “Ukiwa hukosolewi huwezi kutaka maendeleo. Wanaotukosoa kwa nia njema tunawashukuru kwa sababu wanatusaidia kujiridhisha kwenye mambo mengi,” alisema.

Amesisitiza kuwa TFF iko wazi kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali, akieleza kuwa ukosoaji wa kujenga huchochea uwajibikaji na kuboresha utendaji wa taasisi. Kuhusu ushirikiano na Serikali, Karia alisema umeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya TFF, hususan katika utekelezaji wa programu za maendeleo ya vijana.

Ameeleza kuwa mashindano ya shule za msingi na sekondari yanayoandaliwa na Serikali yamekuwa jukwaa muhimu la kutambua vipaji, huku TFF ikivitambua na kuviingiza katika mfumo rasmi wa maendeleo ya soka. Karia amesema mafanikio yanayoonekana katika soka la Tanzania si ya bahati mbaya, bali ni matokeo ya utekelezaji wa mpango mkakati wa shirikisho. SOMA: Mipango inasukwa TFF

Amefafanua kuwa TFF ilitekeleza mpango mkakati wa mwaka 2018 hadi 2022 na baadaye kufanya mapitio yaliyozaa mpango wa mwaka 2023 hadi 2027, unaojumuisha malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu.”Tumetengeneza mpango mkakati. Tulikuwa na mpango wa mwaka 2018 mpaka 2022, baadaye tukafanya mapitio na kuja na mpango wa 2023 mpaka 2027. Kuna mambo ya muda mfupi, wa kati na mrefu na yote tumeyasimamia,” alisema.

Amesema maono ya TFF ni kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye ushindani katika soka katika ngazi zote, jambo ambalo linaanza kudhihirika kupitia mafanikio ya timu mbalimbali za taifa.Kwa mujibu wa Karia, Tanzania imepiga hatua kutoka ushindani wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) hadi kufuzu mara kwa mara mashindano ya Afrika na yale ya Kombe la Dunia katika baadhi ya ngazi za timu za taifa.

Ametaja mafanikio ya timu za vijana, wanawake na timu nyingine za taifa zilizofuzu michuano ya dunia kuwa ushahidi wa matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu katika maendeleo ya soka. Aidha amesema maendeleo hayo yameonekana pia katika ngazi ya klabu, ambapo wawakilishi wa Tanzania wameendelea kushiriki mara kwa mara mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), yakiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..    https://www.work27.info

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button