Kamati yaipongeza Bulyanhulu utekelezaji CSR

SHINYANGA: MGODI wa dhahabu wa Bulyanhulu umetenga na kutumia Sh bilioni 2 kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kurejesha faida kwa jamii (CSR), ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule za msingi na sekondari pamoja na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Evaline Munisi, ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuwa fedha hizo zimetumika katika miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii katika maeneo yanayozunguka mgodi huo.

Munisi amesema hayo leo alipokuwa akiwasilisha taarifa mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Hawa Chikoma, ambapo pia amesema wafanyakazi 7,000 wamepimwa afya zao, huku teknolojia ikitumika katika shughuli za uchimbaji wa madini kwa lengo la kuimarisha usalama wa wafanyakazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Temeke, Mariam Kisangi, ameomba uongozi wa mgodi huo kutoa nafasi zaidi kwa watu wenye ulemavu katika ajira na kuwahusisha katika miradi ya CSR, pamoja na kuwapa elimu kuhusu kanuni za afya na usalama mahali pa kazi.

“Kwa sababu katika taarifa iliyosomwa sijasikia sehemu ambayo imewagusa watu wenye ulemavu. Niwaombe mtupe nafasi watu wenye ulemavu katika CSR mnazofanya na nafasi za ajira katika mgodi huu nasi tuweze kukua kiuchumi,” amesema Kisangi.

Hata hivyo, Meneja wa Mahusiano na Mazingira wa Mgodi wa Bulyanhulu, Agapith Paul, amesema mgodi huo umejenga Shule ya Msingi Segese kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu, huku ikiwekwa mazingira rafiki na vifaa vinavyowawezesha wanafunzi hao kujifunza katika hali ya usalama.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Chikoma, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum, ameridhishwa na utekelezaji wa kanuni za afya na usalama katika Mgodi wa Bulyanhulu uliopo katika Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

“Tunapenda kuona watumishi wote wanajengewa uwezo na wanapatiwa mafunzo ya usalama mahali pa kazi. Pia hongereni kwa kuweka ushirikiano mwema na vyama vya wafanyakazi pamoja na kuona jamii zinanufaika na mgodi,” amesema Chikoma.

Chikoma amesema kamati hiyo inasisitiza kuendelea kushirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuhakikisha taratibu zinafuatwa kama sheria zinavyoelekeza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button