Serikali kuongeza wigo wa utafiti wa madini

GEITA: SERIKALI imejizatiti kuimarisha utafiti wa kina wa jiofizikia kutoka takribani asilimia 16 ya sasa hadi angalau kufikia asilimia 50 ya eneo lote la nchi ifikapo mwaka 2030.
Mpango huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa ambapo hadi mwaka 2025/26 mchango wa sekta ya madini umefikia asilimia 10 huku ikichangia asilimia 56 ya fedha za kigeni.
Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, ametoa taarifa hiyo katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Dk Samia Suluhu mjini Geita.
Dk Kiruswa amesema utafiti wa kina wa jiofizikia utaongeza upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu miamba yenye viashiria vya madini na hivo wizara kuweza kupata maeneo mapya kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

“Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya utafutaji madini inayosababisha wachimbaji wadogo kupoteza mitaji yao”, amesema Dk Kiruswa.
Amesema mpango huo pia ni sehemu ya kutokomeza mila na desturi potofu kwa baadhi ya wachimbaji wadogo ambao awali walikuwa wanafungamanisha uchimbaji wa madini na imani za kishirikina.
“Madini ni sayansi, na sisi kama wizara tumekuja na visiona 2030, kuwaonyesha watanzania ni wapi madini yapo, ya namna gani, yenye ubora gani, kwa kiwango gani ili tukafanye uwekezaji wenye tija”, amesema Dk Kiruswa.

Amesema katika kufangamanisha sekta ya madini na sekta zingine wizara inaendelea kutekeleza Mining for a Better Tommorrow (MBT) ili kuhakikisha madini yananufaisha makundi yote katika kijamii.
Amesema programu hiyo inahusisha utoaji wa nyenzo, msaada wa kitaalamu, utoaji wa taarifa za utafiti, utoaji wa leseni, na fursa zingine za biashara na uwekezaji pamoja na uwendeshaji wa vifaa na mitambo.
Aidha amewahakikishia watanzania wizara inaendelea kufuatilia na kufanyia marekebisho sera na sheria za madini ikiwemo sheria ya hakimiliki aridhi dhidi ya hakimiliki madini ili kupunguza mgongano wa kimaslahi.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amesema ili kuhakikisha madini yanakuwa si chanzo cha migogoro ipo haja kwa wizara ya madini kufanyia mapitio ya sheria ya hakimiliki aridhi na hakimiliki madini.
Mnyeti amesema mpaka sasa kumekuwa na migogoro mingi inayosababishwa na mgongano wa maslahi wa sheria hiyo ambapo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda maslahi ya watanzania.
Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Fredy Liundi amesema kwa mjibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka 2025 mauzo ya madini yalikuwa sh Trillioni 11.7.
Liundi amesema mauzo hayo yanaonyesha usimamizi thabiti wa sekta ya madini chini ya serikali ya awamu ya sita ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo mauzo ya madini yalikuwa takribani Sh Trillioni 7.2.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema kuwa Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini mwaka 2026 yamehusisha washiriki 765 ikiwemo kampuni 15 za uchimbaji wa madini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Ashraf Suryaningrat amepongeza serikali kwa maonyesho hayo na kuyataja kama jukwaa huru na ujuzi, biashara na mahusiano katika sekta ya madini.



