TARURA yaongeza kasi barabara za AFCON Arusha

ARUSHA: Ujenzi wa barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali na Uwanja wa AFCON jijini Arusha umefikia zaidi ya asilimia 60, hatua inayolenga kuboresha usafiri na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka uwanja huo.
Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), unahusisha ujenzi na uboreshaji wa jumla ya kilomita 21.4 za barabara katika maeneo ya Essuri, Lendita na Mateves, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kwa mujibu wa taarifa ya TARURA iliyotolewa Septemba mwaka huu na Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicholas Francis, utekelezaji wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 60, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2027.

Katika eneo la Essuri, mradi unahusisha barabara yenye urefu wa kilomita 2.45 pamoja na ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 100. Barabara ya Lendita yenye urefu wa kilomita 2.75 inajengwa kwa kiwango cha njia nne.
Kwa upande wa Mateves, mradi unahusisha kilomita 6.5, ambapo kilomita 5.5 zitajengwa kwa kiwango cha njia mbili, huku kilomita moja ikijengwa kwa kiwango cha njia nne.
Hatua hiyo inalenga kuboresha muunganiko wa barabara kuelekea Uwanja wa AFCON na maeneo yanayouzunguka, huku miundombinu hiyo ikitarajiwa kuendelea kutumiwa na wananchi na wafanyabiashara hata baada ya kumalizika kwa mashindano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA, Mhandisi Florian Kabaka, amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri, akisisitiza kasi iongezwe katika kazi ambazo hazihitaji matumizi makubwa ya maji kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amesema ziara ya ukaguzi ililenga kutathmini maendeleo ya barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali yanayozunguka Uwanja wa AFCON na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Mbali na mradi wa barabara za kuelekea Uwanja wa AFCON, TARURA ina mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 5,752.834 katika Mkoa wa Arusha, ukiambatana na madaraja 107 na makaravati 2,639 katika wilaya zote sita za mkoa huo.
Kati ya mtandao huo, kilomita 170.407 sawa na asilimia 2.96 ni za lami, kilomita 1,591.267 sawa na asilimia 27.66 ni za changarawe, huku kilomita 3,991.160 sawa na asilimia 69.38 zikiwa za udongo.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TARURA imependekeza bajeti ya takribani Sh bilioni 19.3 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja mkoani Arusha.
Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka uwanja.

Aidha, utekelezaji wa miradi hiyo unatoa fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana wa maeneo yanayopitiwa na barabara, huku miundombinu hiyo ikitarajiwa kubaki kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya jiji hata baada ya AFCON 2027.
Mkazi wa Arusha, Claud Gwandu, amesema maboresho hayo yana umuhimu kwa wananchi kwa kuwa yataendelea kutumika katika shughuli za kila siku hata baada ya kumalizika kwa mashindano.
“Kwa Arusha, matokeo ya uwekezaji huu hayatarajiwi kuishia kwenye maandalizi ya AFCON pekee. Barabara hizi zitabaki kuwa miundombinu ya matumizi ya wananchi, wafanyabiashara na wageni, huku zikisaidia kuunganisha maeneo ya shughuli za kiuchumi na huduma,” amesema.



