Kamati zatakiwa kuwajibika tahadhari ya El Nino

KIGOMA: Serikali imezitaka kamati za maafa katika mikoa na wilaya nchini kuchukua tahadhari mapema dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño, ikiwemo kutambua maeneo hatarishi na kuwaandaa wananchi kuondoka kabla ya maafa kutokea.

Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu, Lina Kitosi, amesema kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kunatoa nafasi ya kupunguza au kuzuia madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.

Kitosi ameyasema hayo wakati akiwasilisha kwa wajumbe wa Kamati ya Maafa Mkoa wa Kigoma mwongozo wa usimamizi na ufuatiliaji wa maandalizi pamoja na taarifa za maafa, ukiolenga kutathmini utayari wa mkoa huo katika kuchukua hatua za kudhibiti na kujikinga na maafa.

Amesema kutokana na tishio la mvua kubwa, kamati za maafa zinapaswa kutambua mapema maeneo hatarishi, kutoa taarifa kwa wananchi wanaoishi mabondeni ili wahame kwa wakati na kutenga maeneo yatakayotumika kama makambi ya muda kwa waathirika.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma na Katibu wa Kamati ya Maafa mkoani humo, Hassan Rugwa, amesema mkoa huo umejiandaa kukabiliana na mafuriko yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Rugwa amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwemo kutoa mafunzo kwa timu za uratibu wa maafa zitakazoshiriki katika kukabiliana na majanga, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari na kuimarisha mifumo ya utoaji na upokeaji wa taarifa.

Amesema pia mkoa umetambua maeneo hatarishi na kutenga maeneo yatakayotumika kuwahifadhi kwa muda wananchi watakaoweza kuathiriwa na mafuriko.

Ameongeza kuwa maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha mkoa unakuwa tayari kuchukua hatua kwa haraka endapo mvua hizo zitasababisha mafuriko au hali nyingine ya hatari.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button