Uhakiki wabaini deni la Sh Bil 1.78 KNCU

KILIMANJARO; Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha na kuinua vyama vya ushirika nchini, kwa lengo la kuhakikisha vinaendeshwa kwa uwazi, uadilifu na uwajibikaji na vinawanufaisha wananchi, hususan wakulima.

Kupitia usimamizi wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Taifa, Serikali imeendelea kutafuta suluhisho la changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika, ikiwemo migogoro, madeni ya muda mrefu, uwajibikaji na uadilifu katika uendeshaji.

Hatua hiyo imeonekana katika Mkutano Mkuu Maalumu wa KNCU ulioitishwa kwa ajili ya kujadili matokeo ya uhakiki wa madeni kati ya KNCU na vyama wanachama, ambapo uhakiki huo uliofanywa na COASCO umebaini kuwa KNCU inadaiwa jumla ya Sh1,782,919,016.

Uhakiki huo umehusisha kipindi cha miaka 14 ya fedha hadi mwaka 2024/25, huku vyama 92 vya msingi vikiwa wanachama wa KNCU.

Kati ya hivyo, vyama 84 vilishiriki katika zoezi hilo, ambapo 64 vilibainika kuwa na madai dhidi ya KNCU, huku vyama vinne vikiwa na madeni kwa KNCU. Vyama vinane havikushiriki uhakiki huo.

Akizungumza kwenye mkutano huo jana, Mrajis wa Vyama vya Ushirika Taifa, Dk Benson Ndiege, amesema uhakiki huo umeweka wazi kiwango cha deni kinachoweza kuthibitishwa kwa nyaraka, lakini bado kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina, ili kubaini chanzo cha madeni na hasara zilizojitokeza katika kipindi cha nyuma.

Amesema Mkutano Mkuu Maalumu umeafiki kufanyika kwa uchunguzi wa kiforensiki (forensic investigation), ili kubaini chanzo cha madeni hayo, pamoja na iwapo kuna watendaji au viongozi waliowahi kuhusika.

“Tumekubaliana kufanya uchunguzi maalumu wa kina, ili kuangalia uhalisia wa jambo hili. Ingawa miaka mingi imepita, tutafikia kiini cha tatizo na wahusika watawajibishwa kwa mujibu wa nyaraka na sheria,” amesema Ndiege.

Amesema uchunguzi huo unalenga pia kubaini iwapo madeni hayo yalisababishwa na mdororo wa kiuchumi, hasara za biashara, au hatua na maamuzi ya watendaji na viongozi waliowahi kusimamia KNCU huko nyuma.

Kwa mujibu wa taarifa ya uhakiki, kati ya vyama 84 vilivyoshiriki, vyama 64 vilibainika kuwa na madai dhidi ya KNCU, huku vyama vinne vikibainika kuwa na madeni kwa KNCU. Pia, chama kimoja kilikuwa na madai ya takribani Sh 8 milioni.

Uhakiki huo ulifanyika kwa hatua mbalimbali, ikiwemo kufanya vikao na KNCU, kuchambua nyaraka, kulinganisha kumbukumbu za KNCU na zile za vyama wanachama, kupitia madai ya pande zote mbili na kufanya mahojiano na vyama husika.

Katika madai yaliyohusisha miradi ya pamoja, ripoti imebainisha kiasi cha takribani Sh24 milioni, sawa na takribani Sh 6 milioni kwa kila mradi wa pamoja.

Ndiege amesema changamoto kubwa katika kazi hiyo ilikuwa upatikanaji wa nyaraka za zamani. Baadhi ya nyaraka hazikuweza kupatikana, huku mabadiliko ya mara kwa mara ya watendaji yakisababisha baadhi ya kumbukumbu kupotea au kukosekana kwa watu wenye uelewa wa historia ya miamala hiyo.

Pia, baadhi ya nyaraka zilichelewa kuwasilishwa au hazikuwasilishwa kabisa na vyama husika.

Amesema tofauti zilizokuwepo kati ya kumbukumbu za KNCU na madai ya vyama wanachama ndizo zilizofanya zoezi la reconciliation kuwa muhimu katika kubaini deni linaloweza kuthibitishwa kwa nyaraka.

Kuhusu hatua zinazofuata, Ndiege amesema KNCU itaunda timu maalumu itakayopendekeza namna ya kulipa madeni yaliyothibitishwa, kisha mapendekezo hayo yatawasilishwa mbele ya wanachama kwa ajili ya kujadiliwa na kuafikiwa.

“Deni lipo na ni lazima lilipwe. Kinachotakiwa sasa ni kuweka utaratibu wa malipo na kuhakikisha unatekelezwa,” amesema.

Amesema serikali inaendelea kutumia ushirika kama nyenzo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kuendeshwa kwa misingi ya uadilifu, uwazi na uwajibikaji.

Aidha, amesema serikali inaendelea na taratibu za kuboresha vyama vya ushirika kupitia kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, inayolenga kutafuta majawabu ya changamoto zinazofanya vyama hivyo visifanye vizuri.

Kuhusu migogoro ya mali na mashamba, Ndiege amesema kati ya migogoro 19 iliyokuwepo, 16 imeshughulikiwa na mitatu imebaki ikiendelea kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Vijijini, Enock Koola, amesema uhakiki huo ni hatua muhimu katika kuweka wazi ukweli kuhusu madeni yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya KNCU na vyama vya msingi.

Amesema yeye pamoja na Mbunge Morris Makoi waliwasilisha hoja na kufanya mahojiano kuhusu madai ya wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika ambao wamekuwa wakisubiri malipo yao kwa muda mrefu.

Koola amesema baada ya mahojiano hayo, Mrajis aliahidi kuunda kamati mbalimbali na kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika kutoka Moshi Vijijini na Vunjo wanapata haki yao.

Amesema uhakiki huo umewezesha kupata uelewa mpana kuhusu kiwango cha deni kinachoweza kuthibitishwa, huku akisisitiza kuwa mchakato huo haupaswi kuishia kwenye ripoti pekee.

Koola amesema anaunga mkono uamuzi wa kufanya uchunguzi wa kiforensiki, ili kubaini chanzo cha madeni na hasara zilizojitokeza, na iwapo uchunguzi utabaini ukiukwaji wa taratibu, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

“Kwa upande wangu, nimejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanapata haki yao. Tutaunga mkono mchakato huo na tutafuatilia hatua kwa hatua ili kuhakikisha haki inatendeka,” amesema.

Amesema iwapo uchunguzi utabaini kuwa kuna viongozi au watendaji wa KNCU ambao hawakutenda kwa uadilifu na kusababisha hasara, vyombo husika vinapaswa kuwabaini na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria.

“Fedha zilizopotea zinapaswa kurejeshwa na waliohusika wawajibishwe. Hata hivyo, jambo la msingi zaidi kwa sasa ni kuhakikisha wakulima wa Vunjo na Moshi Vijijini wanapata haki yao,” amesema.

Koola amesema wabunge wataendelea kufuatilia suala hilo bungeni na kwa waziri mwenye dhamana, ili kuhakikisha hatua zilizokubaliwa zinatekelezwa na madeni yaliyothibitishwa yanafanyiwa utaratibu wa malipo.

Naye Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, amesema mkutano huo ulikuwa muhimu kwa sababu umeweka wazi madai ya vyama vya msingi na kutoa msingi wa kuendelea kutafuta suluhisho la changamoto hiyo.

Amesema wakulima wamekuwa wakisubiri malipo yao kwa muda mrefu na kwamba kuchelewa kwa malipo hayo kunaathiri maisha yao pamoja na uzalishaji wa kahawa.

Ameiomba serikali na uongozi wa KNCU kuhakikisha mpango wa kulipa madeni yaliyothibitishwa unaandaliwa na kutekelezwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Amesema hatua iliyofuata inapaswa kuwa kuhakikisha matokeo ya uhakiki na uchunguzi yanafanyiwa kazi, huku wakulima wakiendelea kupewa taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button