Kituo kipya kuongeza huduma za meno

DAR ES SALAAM: Huduma za afya ya kinywa nchini zinatarajiwa kuimarika baada ya Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam kuzindua kituo maalumu cha huduma za meno na vipandikizi vya meno, katika hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa.

Kituo hicho kimejengwa kwa uwekezaji wa Sh bilioni 1.3 na kina vyumba sita vya kisasa vyenye vifaa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za meno, ikiwemo huduma za vipandikizi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Emmanuel Tayari, amesema uwekezaji huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya, ambapo takribani asilimia 85 ya huduma za afya katika Mkoa wa Dar es Salaam hutolewa na sekta hiyo, huku katika huduma za afya ya kinywa ikifikia asilimia 70.

Tayari amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za afya ya kinywa kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa, radiolojia ya meno kwa njia ya kidijitali pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma hizo.

Amesema mkazo pia umewekwa katika kinga, utambuzi wa mapema na matibabu kwa wakati ili kupunguza hali ya wagonjwa kusubiri hadi kung’oa jino kuwa suluhisho pekee.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya mifumo ya bima ya afya na hospitali binafsi unaendelea kuimarika, akitolea mfano Hospitali ya Aga Khan ambayo hivi karibuni ilisaini mkataba na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wa kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Profesa Muzdalifat Abeid, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza huduma maalumu za afya zenye viwango vya juu, kwa lengo la kupunguza idadi ya Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Utafiti wa Kitaifa wa Afya ya Kinywa wa mwaka 2020 ulionesha kuwa asilimia 76 ya Watanzania watu wazima waliathiriwa na tatizo la kuoza kwa meno, huku asilimia 52 wakiwa na ugonjwa wa fizi.

Aidha, hadi Julai 2025, ni asilimia 42 pekee ya vituo vya afya vya umma vilivyokuwa vikitoa huduma za afya ya kinywa, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa huduma hizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button