Mfanyabiashara atoa msaada wa chakula

Mfanyabiashara Dennis Steven maarufu kwa jina la King Papaa, amekutana na mashehe, walimu wa madrasa na viongozi wasaidizi wa misikiti katika Kata ya Kimara, Dar es Salaam, na kuwapatia msaada wa chakula ikiwa sehemu ya sadaka na jitihada zake za kusaidia jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, King Papaa alisema ametoa tani moja na kilo 400 za mchele pamoja na tani moja na kilo 400 za unga, akieleza kuwa msaada huo unalenga pia kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
“Nimeona sadaka yangu pia iwe sehemu ya chakula,” alisema King Papaa.
Alisema ameamua kuwasaidia viongozi hao kutokana na mchango wao katika kueneza mafundisho ya dini na kujenga jamii yenye maadili.
King Papaa pia aliwataka wafanyabiashara, viongozi wa Serikali, wabunge na madiwani kutumia sehemu ya walichojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwasaidia wananchi, badala ya kuwakumbuka wakati wa kampeni pekee.
Aidha, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuwaelimisha waumini kuhusu tahadhari zinazotolewa na Serikali kuhusu mvua za El Niño, akisema misikiti na maeneo mengine ya ibada ni sehemu muhimu ya kuwafikia wananchi kwa taarifa zinazohusu usalama wao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BAKWATA Kata ya Kimara, Khamis Rashid, alimpongeza King Papaa kwa msaada huo, akisema umeonyesha huruma na kujali jamii. Aliwataka watu wenye uwezo kuiga mfano huo kwa kusaidia wenye uhitaji.
Naye mkazi wa Kimara, Abdull Aziz, alisema King Papaa amekuwa akitoa misaada katika eneo hilo mara kadhaa, akieleza kuwa ameshafanya hivyo zaidi ya mara tatu au nne.
Abdull alisema King Papaa ni mfano kwa vijana kutokana na kujitolea kwake kusaidia jamii. Alitoa mfano wa tukio ambalo mfanyabiashara huyo alimchangia mama mmoja kiasi cha shilingi 500,000 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wake kupata sare za shule.
Kwa upande wao, waliopokea msaada huo walimshukuru King Papaa kwa kuendelea kuunga mkono jamii ya Kimara, wakisema msaada wake umekuwa ukitolewa mara kadhaa katika maeneo mbalimbali.



