Wageni wavutiwa uwekezaji AFCON 2027

DAR ES SALAAM; Tanzania imeanza kutumia maandalizi ya mashindano ya AFCON kama fursa ya kujitangaza kimataifa, ikilenga kuvutia watalii na wadau wa michezo kupitia wageni kutoka nje wanaotembelea nchini.
Mkakati huo umejidhihirisha baada ya kundi la waandishi wa habari, watu mashuhuri na watengeneza maudhui kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Tanzania kwa ajili ya kushuhudia maandalizi ya mashindano hayo na kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii.
Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nassor Garamatatu, amesema ziara hiyo inalenga kuwapa wageni hao fursa ya kuifahamu Tanzania kwa karibu ili baadaye watumie vyombo vyao vya habari na majukwaa ya kidijitali kuitangaza nchi katika masoko ya kimataifa.
Amesema uwekezaji uliofanyika katika miundombinu ya michezo, ukiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uwanja wa Gymkhana, ni miongoni mwa maeneo yanayolenga kuonyesha uwezo wa Tanzania kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.

“Mbali na Dar es Salaam, kundi hilo linatarajiwa kutembelea Arusha na Fumba, Zanzibar, likilenga kujionea vivutio vya utalii na maandalizi ya AFCON,” amesema Garamatatu.
Kwa upande wake, mwandishi wa habari na mtengeneza maudhui kutoka Ufaransa, Alizee Morat, amesema ziara hiyo imembadilishia mtazamo kuhusu Tanzania, akieleza kuvutiwa na maendeleo ya miundombinu pamoja na ukarimu wa Watanzania.
“Sikufikiri Tanzania kuwa ni ya kisasa kiasi hiki,” amesema Alizee, ambaye amewahi kutembelea nchi nyingine za Afrika, ikiwemo Cameroon.
Kiongozi wa msafara huo, John Jackson, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kutumia AFCON kama fursa ya kuwaunganisha wageni na vivutio vya Tanzania, ili wawe mabalozi wa kuitangaza nchi kupitia mitandao na majukwaa yao mbalimbali.
Jackson amesema wamevutiwa pia na Uwanja wa Benjamin Mkapa, akieleza kuwa uwekezaji uliofanyika katika uwanja huo unaweza kulinganishwa na viwanja vikubwa duniani.
Kwa Tanzania, hatua hiyo inaongeza wigo wa kuitumia michezo si kwa ajili ya ushindani pekee, bali pia kama nyenzo ya kutangaza utalii, miundombinu na fursa za uwekezaji kwa hadhira ya kimataifa.



